UONGOZI wa Yanga umebainisha kuwa watafanya kazi kubwa kwenye mechi za kitaifa na kimataifa malengo ikiwa ni kufanya vizuri kutokana na uimara wa wachezaji wao.
Yanga kwenye dirisha dogo la usajili ilitambulisha wachezaji wapya watatu ambao ni Agustino Okra, Shekhan Ibrahim na Joseph Guede.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kwenye kila mashindano ambayo wanashiriki ushindani ni mkubwa jambo ambalo linawafanya wazidi kujiimarisha.
“Ipo wazi kwamba inahitajika kazi kubwa na jitihada kufikia malengo kutokana na ushindani uliopo kwenye kila idara hilo tunalitambua kwani ligi yetu ni miongoni mwa ligi bora.
“Mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi kwenye mechi zilizopo na muda upo kwa ajili ya maandalizi yanayofuata kitaifa na kimataifa kwa kuwa ushindi unapatikana uwanjani kwa wachezaji kujituma na kufanya kazi yao kuwapa burudani mashabiki ndani ya uwanja,” amesema Kamwe.