AHMED Ally ambaye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, anatamani Mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) yamalizike hata leo ili waanze kuona ubora wa washambuliaji wao wapya waliowasajili juzi kabla ya dirisha dogo kufungwa la msimu huu.
Simba juzi iliwatangaza washambuliaji wawili Fredy Michael Koublane na Pa Omar Jobe ambao wametambulishwa saa chache kabla ya usajili kufungwa juzi.
Wakiwasajili nyota hao, haraka walitangaza kuachana na washambuliaji wake Moses Phiri na Jeane Baleke aliyerejeshwa katika klabu yake ya TP Mazembe ya DR Congo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Ahmed alisema kuwa washambuliaji hao wote waliowasajili ni mapendekezo ya kocha wao Mualgeria, Abdelhak Benchikha ambao anafahamu ubora wao kabla ya kuwapa mikataba ya kuichezea timu hiyo.
Ahmed alisema kuwa wao viongozi wanatamani mashindano ya Afcon imalizike mapema, kwa lengo la mashabiki kupata burudani ya mabao mazuri yatakayofungwa na washambuliaji hao wenye viwango bora.
Aliongeza kuwa mabeki wa timu pinzani wajiandae kupata ushindani mkubwa kutoka kwa washambuliaji hao huku akiwataka mashabiki kujiandaa kushangilia mabao hadi wachoke wenyewe.
“Hizi mashine mbili tulizozitambulisha juzi jana (juzi) saa chache kabla ya dirisha dogo kufungwa, zinajua kufunga mabao hatari ambao mabeki watakuwa dhaifu, basi watakiona.
“Hiyo inatupa ujasiri Viongozi wa kutamani Afcon imalizie hata leo, ili mashabiki wapate burudani ya kushangilia mabao watakayoyafunga sambamba na kupata burudani yao ya soka, kwani washambuliaji hao wanalijua boli.
“Wote hao ni pendekezo la kocha Benchikha, tunaamini ujio wa washambuliaji utaongeza kitu katika timu, kutokana na ubora wao waliotoka nao katika timu zao wakiwa wanacheza katika viksi vya kwanza,” alisema Ahmed.