HUKU zikiwa zimesalia siku sita kabla ya kufungwa kwa doirisha dogo la usajili wa timu zilizo chini ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ametangaza kuwa ametumia mashindano ya Kombe la Mapinduzi kufanya tathimini ya kikosi chake na sasa kuna maamuzi mazito yatatolewa hivi karibuni.
Yanga imeondolewa katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo, kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya APR ya nchini Rwanda mchezo uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Aman Complex, Zanzibar.
Kocha huyo katika mashindano hayo, aliwapa nafasi ya kucheza wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kucheza katika Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika na vijana wa U20 waliowapandisha kwa ajili ya kutathimini vwango vyao kabla ya kuchukua maamuzi ya kuwakata katika dirisha dogo.
Kupitia dirisha dogo la usajili yanga imefanikiwa kukamilisha usajili wa mastaa wawili na kuwatangaza mpaka sasa ambao ni, Shekhani Ibrahim na kiungo wa kimataifa wa Ghana, Augustine Okrah huku wakielezwa kuwa kwenye hatua za mwisho za kushusha mshambuliaji wa kimataifa.
Yanga wanatarajiwa kuachana na straika, Hafiz Konkoni ambaye ameshindwa kupata nafasi kwenye kikosi hicho chini ya kocha mkuu, Miguel Gamondi.
Akizungumza na Championi Jumatano, Gamondi alisema kuwa malengo ya kushiriki mashindano hayo, yametimia kwa kiwango kikubwa ambayo ya kwanza yalikuwa ni kuwatambua wachezaji wachezaji wasiokuwa na sifa ya kubakia kuendelea Yanga.
Aliongeza kuwa amepanga kukabidhi ripoti ya wachezaji hao kwa uongozi, hivi karibuni ikiwa ni siku chache tangu watoke kuondolewa katika mashindano hayo.
“Licha ya kuondolewa katika hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Mapinduzi, lakini kwangu nimefurahia kuona malengo ya ushiriki wa mashindano haya kukamilika.
“Malengo yangu yalikuwa ni kuwapa nafasi ya wachezaji wale wa benchi ambao hawakupata nafasi nyingi ya kucheza katika ligi na michuano ya kimataifa kuwatumia kwa ajili ya kutathimini kiwango cha kila mmoja kabla ya kuchukua maamuzi ya kutoa mapendekezo ya kuwaacha na wengine kuwabakisha.
“Hivyo malengo yangu yametimia, na kinachofuata hivi ni utekelezaji wa viongozi baada ya mimi kukamilisha ripoti yangu,” alisema Gamondi.