BENCHIKHA AMVUTA MBADALA WA CHAMA SIMBA

KOCHA Mkuu wa Simba, Mualgeria, Abdelhak Benchikha, amewasilisha jina la kiungo wa zamani wa Paide Linnameeskond ya nchini Estonia, Babou Cham raia wa Gambia kwa ajili ya kuwa mbadala wa Clatous Chama.

Benchikha tayari amewasilisha orodha ya wachezaji anaowahitaj kwa ajili ya kuongezwa katika dirisha dogo kati ya hao, yupo kiungo mkabaji Babacar Sarr aliyetambulishwa hivi karibuni.

Kocha huyo anaendelea kukiboresha kikosi chake kwa kuongeza maingizo mapya katika dirisha dogo, kati ya hao amebakisha mshambuliaji pekee baada ya kumpata kiungo mkabaji na huyo mshambuliaji ambaye amependekeza asajiliwe.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, licha ya ugumu wanaoupata Simba wa kuipata saini ya kiungo huyo mwenye uwezo wa kutokea kulia na kushoto, lakini uongozi wa klabu hiyo umeahidi kupambana kuipata saini ya nyota huyo.

Mtoa taarifa huyo alisema dili hilo lipo katika hatua za mwisho kukamilika, kutokana na mazungumzo yanayoendelea kati ya menejimenti ya mchezaji huyo na Simba.

Aliongeza kuwa, kiungo huyo anakuja kuchukua nafasi ya Chama ambaye, inaelezwa Kocha Benchikha amemuondoa katika mipango yake ya msimu huu kwa kile kilichotajwa utovu wa nidhamu.

“Asilimia kubwa ya wachezaji ambao wametambulishwa baada ya usajili wao kukamilika katika dirisha dogo, wote ni mapendekezo ya Kocha Benchikha ambaye aliwasilisha majina yao.

“Kati ya hao yupo kiungo mshambuliaji mwenye uwezo wa kutokea kulia na kushoto raia wa Gambia, anaitwa Babou Cham, jina lake limependekezwa na kocha ambaye anakuja kuchukua nafasi ya Chama.

“Chama ni kati ya wachezaji ambao kocha amewaondoa katika mipango yake, hivyo kama taratibu zikikamilika basi tutamsajili katika dirisha hili dogo,” alisema mtoa taarifa huyo.

Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Usajili uliokamilika ndiyo tunauweka wazi, kwa sasa jina la huyo kiungo mpya bado halijafika mezani kwangu, lakini kikubwa ifahamike kuwa suala la usajili lote lipo chini ya kocha ambaye viongozi hatutamuingilia.”

Rekodi zinaonesha kwamba, nyota huyo kwa sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Paide kumalizika, huku akiwa amewahi kucheza Nomme United ya Estonia, Ararat Yerevan (Armenia), SC Noravank (Armenia), FC Sevan (Armenia) na Real de Banjul ya kwao Gambia.