YANGA YAJIVUNIA JEMBE HILI LA KAZI

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa una kila sababu za kujivunia uwepo wa wachezaji wao wote wanaofanya kazi kwa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kiungo Aziz KI.

Ikumbukwe kwamba Aziz KI ni namba moja kwenye utupiaji ndani ya ligi akiwa na mabao 10 kibindoni sawa na namba ya jezi yake pendwa mgongoni akiwa uwanjani kutimiza majukumu yake.

Bao la 10 alifunga kwenye mchezo wa mwisho ndani ya 2023 dhidi ya Tabora United mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na ubao ulisoma Tabora United 0-1 Yanga.

 Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema kuwa wana wachezaji wengi wanaofanya vizuri jambo ambalo linafanya wajivunie uwepo wao.

“Kuna wachezaji wanaofanya kazi kubwa uwanjani wote kwa ushirikiano hilo ni muhimu. Hata anayeongoza kwa kufunga sio mshambuliaji kama ambavyo wanasema lakini anatoka Yanga hilo lipo wazi.

“Ikiwa ipo hivi basi nao wanaotusema watuambia mshambuliaji wao yuko wapi na kipi ambacho kinafanyika. Hakuna namna ni lazima tuwapongeze wachezaji wetu wanafanya kazi kubwa kutimiza majukumu yao,” alisema Kamwe.