INAELEZWA mabosi wa Simba wapo kwenye mazungumzo na winga wa klabu ya Sporting Lagos ya Nigeria, Jonathan Alukwu kufuatia maagizo ya kocha mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha katika usajili wa dirisha dogo.
Taarifa za uhakika zilizotufikia Championi Ijumaa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa klabu hizo mbili zimeanza mazungumzo hayo na nyota huyo ambaye amepewa kipaumbele kuchukuwa nafasi ya Saidi Ntibazonkiza.
Mtoa taarifa aliongeza kuwa, hatua ya kuwania saini ya nyota huyo ni baada ya Saido Ntibazonkiza huenda akaondoka Simbazi na kwenda klabu ya APR ya Rwanda katika usajili huu wa dirisha dogo.
“Skauti ya Simba na benchi la ufundi la kocha Benchikha imeridhika Alukwu, kwa kuwa mwalimu anafahamu uwezo wake na endapo watafanikiwa kumpata watakuwa wamefanikiwa kuziba nafasi ya Saido ambaye muda wowote akaondoka,” alisema mtoa habari huyo.
Aliongeza kuwa viongozi wanakamilisha masuala ya usajili kulingana na mapendekezo ambayo wameyapokea kutoka kwa benchi hilo la ufundi linaloongozwa na Benchikha.
Championi Ijumaa lilimtafuta Meneja wa Habari na Mawasiliano ya Simba, Ahmed Ally azungumzie ishu hiyo ambapo alisema suala zima la usajli wa timu hiyo kwa sasa limebakia kwa kocha mkuu wa timu hiyo ndiyo anaweza kuamua wachezaji anaowataka ndani ya kikosi chake.
Dirisha dogo la usajili limefunguliwa Desemba 15, mwaka huu na utafungwa Januari 15, mwakani.