BAADA YA HAT TRICK YA AZIZ KI… SIMBA: HATUNA HOFU, KIATU NI CHA BALEKE

UONGOZI wa Simba umebainisha kuwa kwa namna wachezaji wao walivyo na shauku ya kufunga mabao mengi kwenye kila mechi wanazocheza ndani ya ligi wana imani tuzo ya kiatu bora itakuwa kwenye mikono yao msimu wa 2023/24.

Kauli hiyo ni kama kumpora kiatu cha ufungaji bora mwamba Aziz Ki ambaye kwa sasa ni kinara wa utupiaji akiwa na mabao sita kibindoni baada ya kucheza mechi sita.

Ikumbukwe kwamba msimu wa 2022/23 ni Fiston Mayele wa Yanga na Saido Ntibanzokiza wa Simba walikomba tuzo hiyo baada ya wote wawili kutupia kambani jumla ya mabao 17.

Mayele hayupo ndani ya Bongo yupo zake Misri katika Klabu ya Pyramids huku Ntibazonkiza akiwa ndani ya Simba akiendelea kupambania kombe akiwa katupia mabao mawili.

Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally alisema kuwa kuna uwezekano mkubwa kiatu cha ufungaji bora kikawa mikononi mwa Jean Baleke.

“Unaiona kasi ya mshambuliaji Jean Baleke kwenye kufunga mabao jinsi ilivyo? Haishangazi hii ni kazi anayoipenda na usisahau kuwa ana hat trick aliyoifunga kwenye Uwanja wa Uhuru dhidi ya Coastal Union.

“Waanze kumuandalia kiatu cha ufungaji bora mabao matano sasa, ana kasi, uwezo na anapenda kufunga akiwa langoni hivyo huu ni mwanzo mwisho unakuja watafurahi zaidi,” alisema Ally.