UNYAMA unatarajiwa kuendelezwa leo nchini Misri kwa mchezo wa hatua ya robo fainali ya pili ya African Football League kati ya Al Ahly dhidi ya Simba kutoka Tanzania.
Benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira limebainisha kuwa lina imani ya kupata matokeo ugenini ili kutinga hatua ya nusu fainali.
Hapa tunakuletea hesabu namna ilivyo kwa wawakilishi hawa wa Tanzania kimataifa:” “Kupata sare nyumbani ni matokeo ambayo hatukutarajia tulihitaji ushindi. Tunawafuata kwao na tunaamini tutapata ushindi.
Haya ni baadhi ya maneo ambayo Simba wanapaswa kuyafanyia kazi kutusua mbele ya Waarabu hao wa Misri ukiweka kando umakini kwenye kumalizia nafasi wanazopata na viungo kucheza kwa kushirikiana mengine yapo hivi:-
Ukuta wa Yeriko unavunjika
Ule ukuta wa Simba ambao ulipewa jina la ukuta wa Yeriko unavunjika kwenye kila mechi za kimataifa inazocheza. Kazi kubwa itakuwa kwenye kuboresha eneo hilo kutokana na kuruhusu makosa mara kwa mara.
Ikumbuwe kwamba kwenye hatua ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika mechi mbili ambazo ni dhidi ya Power Dynamos ilitunguliwa mabao matatu. Mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya African Football League dhidi ya Al Ahly ni mabao mawili yalizama nyavuni Uwanja wa Mkapa.
Che Malone Fondoh, Henock Inonga hawa ni mabeki wa kati wa Simba huku Mohamed Hussein na Shomari Kapombe hawa ni mabeki wa pembeni wana kazi kuongeza umakini kuelekea mchezo huo.
Oliveira amesema kuwa ni muhimu ulinzi kuwa bora kwenye mechi zote wanazocheza ili kupata ushindi.
“Mechi zote kwetu ni muhimu kuwa makini kwenye ulinzi hiyo itaongeza hali ya kujiamini pale tunapopata bao. Makosa yapo na hayo tunayafanyia kazi kwa kuwa mchezo wa mpira ni mchezo wa makosa.
Mikato ya kimyakimya ndani ya 18
Mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali uliochezwa Uwanja wa Mkapa ilibaki kidogo Al Ahly wapate penalti kutokana na mikato ya kimyakimya iliyofanywa na beki wa Simba, Henock Inonga dakika ya 34. Matumizi ya teknolojia ya VAR yaligomea penalti hiyo.
Kazi ni kubwa kwa Simba kuongeza makini ugenini, Al Ahly wakiwa na jambo lao ni ngumu kuwazuia kwa wepesi. Hata bao la pili ambalo Simba walifungwa dakika ya 63 lilitokana na tafsiri ya mwamuzi kuwa nyota wa Simba alicheza faulo na pigo hilo likatibua rekodi ya kupata ushindi nyumbani.
Robo fainali inatosha
Kushiriki kwenye mashindano makubwa Afrika inaonesha kuwa mafanikio makubwa ya Simba ni kugotea hatua ya robo fainali. Hata msimu wa 2022/23 waligotea hatua hiyo walipofungashiwa virago na Wydad Casablanca kwa penalti.
Inatosha kwa Simba kugotea hapo hivyo kazi kubwa kwa wachezaji iwe kupambania kuvunja rekodi hiyo na kutinga hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza kwenye michuano hii mipya.
Makipa pasua kichwa
Licha ya kuwa na makipa wenye uzoefu mkubwa ikiwa ni pamoja na Ayoub Lakred, Ally Salim bado wote makosa yao yanafanana kila wakipewa nafasi ya kuanza.
Kuumia kwa Aishi Manula ambaye ni kipa namba moja wa Simba kunaivuruga timu hiyo kukosa chaguo sahihi la nani atakayetimiza majukumu kwa umakini.
Salim ni kipa mzuri lakini kwenye mechi kubwa za kimataifa anaonekana kutozungumza na safu yake ya ulinzi na namna ya uokoaji wa hatari akiwa ndani ya 18 kuwa faida kwa wapinzani.
Lakred anaonekana kuwa mzito kwenye maamuzi ya haraka na ile mipira ya mbali bado hajawa imara hivyo kuna umuhimu wa benchi la ufundi kuyafanyia kazi haya.