MVURUGANO wa mipango hutibua mengi yanayotarajiwa kufanyika. Kufungashiwa virago katika anga la kimataifa kuliwarudisha chini na kuanza kujipanga upya kwa wakati ujao.
Matajiri wa Dar, Azam FC wanazidi kujitafuta katika kuonyesha falsafa yao ya bidhaa bora, timu bora ndani ya Ligi Kuu Bara.
Hasheem Ibwe, Ofisa Habari wa Azam FC ameweka wazi kuwa hesabu kubwa ni kuwa na mwendelezo mzuri kwenye kila mechi ambazo wanacheza.
“Timu kubwa inafanya makubwa, kwenye mechi ambazo tunacheza tumedhamiria kuwa na matokeo bora na kupata pointi tatu muhimu,”.
Hapa tunakuletea namna kazi inavyopigwa na wapambanaji hao:-
Mitambo ya mabao
Prince Dube
Muuaji anayetabasamu, Prince Dube anauwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao akiwa uwanjani. Alifungua akaunti yake ya mabao kwenye mchezo dhidi ya Tabora United dakika ya tano Uwanja wa Azam Complex.
Kibindoni ana mabao mawili na pasi moja ya bao alitoa kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons ilikuwa dakika ya 47 akiwa ndani ya 18. Aliwafunga pia Prisons bao la pili dakika ya 11, Agosti 28.
Feisal
Ni kinara wa utupiaji mabao akiwa nayo manne, matatu alifunga mchezo dhidi ya Tabora United, Ni mchezaji wa kwanza kufunga ndani ya Azam FC na kete yake ya nne aliwatungua Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mapigo huru
Cheikh Sidibe ni mtaalamu wa kazi za mapigo huru ndani ya Azam FC. Kibindoni ana bao moja aliwatungua Singida Fountain Gate ilikuwa Uwanja wa Azam Complex kwa pigo huru. Kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union alipewa majukumu hayo pia kama ambavyo alifanya dakika ya 6.
Kipa la mpira
Idrisu Abdulai huyu ni chaguo la kwanza chini ya Kocha Mkuu, Yusuph Dabo. Ni mechi zote tano alianza kikosi cha kwanza akikomba dakika 450. Hajafungwa kwenye mechi tatu ambazo ni dakika 360.
Mechi mbili kakutana na joto ya jiwe kwa kutunguliwa bao mojamoja ilikuwa mchezo dhidi ya Tanzania Prisons na Singida Fountain Gate zote zilichezwa Uwanja wa Azam Complex.
Jasho lilimwagika
Ni kivumbi ilikuwa kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Dodoma Jijiwalipokuwa ugenini. Wakulima wa zabibu walionyesha ushindani mkubwa na kuwa moja ya mchezo uliomwaga jasho kwa wapinzani wote.
Ngoma ilipigwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Oktoba 3,2023 ubao ukasoma Dodoma Jiji 0-0 Azam FC wote wakakomba pointi mojamoja.
Jioni kabisa waliambulia kicheko
Ule usemi wa usimkatie mtu tamaa ulijibu kwenye mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate. Wakati ngoma ikiwa inakaribia kugota mwisho, jioni kabisa bao la ushindi likajazwa kimiani.
Ni Idd Suleiman, (Nado) Septemba 21 alipachika bao la ushindi kwa pigo la kichwa ilikuwa dakika ya 90+2. Ubao ukasoma Azam FC 2-1 Azam FC pointi tatu zikabaki ndani ya Uwanja wa Azam Complex.
Kigongo kijacho
Wamerejea chimbo kuwawinda Yanga Oktoba 25 mchezo wa Dabi ya Mzizima. Ni mara ya pili kukutana kwa timu hizi mbili ndani ya 2023.Kete ya kwanza ilipigwa kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, Tanga Uwanja wa Mkwakwani ubao ukasoma Yanga 2-0 Azam FC.
Kete ijayo itakuwa ni msako wa pointi tatu ndani ya dakika 90. Kwenye msimamo Azam FC ipo nafasi ya pili na pointi 13 Yanga nafasi ya tatu na pointi 12.