TUNA INFANTINO, MOTSEPE,KWA MKAPA, TUWAPE UJUMBE SAHIHI

SIMBA wanashiriki michuano ya African Football League ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza katika historia ya mpira wa Afrika.

Simba ndio timu pekee kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki ambao wanakuwa wawakilishi katika ukanda huo.

Si jambo dogo, tunapaswa kujivunia sana kwa kuwa majirani zetu kama Kenya, Uganda, Rwanda na wengine wangetamani sana kufikia hapo tulipo.

Wangetamani kuwa na timu ambayo iko katika hatua hiyo kwa kuwa wanajua heshima ya michuano hiyo mikubwa ikiwa ndio inaanza kwa mara ya kwanza katika historia ya mpira wa Afrika.

Jambo hili kama linachukuliwa kishabiki na ushindani wa Simba na Yanga, imekuwa ikilazimishwa lionekane kama ni jambo la kawaida sana.

Badala ya kuonekana ni jambo la kujivunia na kwa kuwa hakuna upande wa Simba au Yanga ungependa mwenzake kuwa na jambo la kujivunia.

Walichokifanya Simba, kinatamaniwa na klabu zote za Tanzania lakini ukanda wote wa Afrika Mashariki. Si kwa kuwa wamepata fedha nyingi, si kwa kuwa watacheza na Al Ahly lakini ni kwa kuwa wanaingia kwenye rekodi kubwa ya kuanza kwa michuano hiyo ikiwa ni timu ya kwanza ya Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki.

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino atakuwa moja ya wageni siku hiyo kwenye Uwanja wa Mkapa kama itakavyokuwa kwa Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (Caf), Patrice Motsepe.

Tuna Infantino jukwaani kwa Mkapa, tuna Motsepe pia, kuna nini tena katika mpira. Hii ni rekodi kuwa na marais hawa wakubwa wawili wakishuhudia mechi ya timu ya Tanzania ikicheza dhidi ya kigogo wa Afrika na moja ya timu zinazomiliki makombe mengi kwenye kabati lake la makombe, Al Ahly.

Tunaweza kuwapa ujumbe maridadi sana Marais hawa wawili wa mashirikisho makubwa ya soka kwa kuwaonyesha tunaweza kwenye mengi kuliko walivyotarajia.

Kwanza ni lazima kuujaza uwanja, lakini ni lazima kuwaonyesha kuwa Watanzania pamoja na kuujaza uwanja, wanaweza kushangilia kwa amani mwanzo mwisho.

Tuwaonyeshe tunaweza kushangilia na kwetu mpira ni sehemu ya upendo. Sehemu ya kuungana na kufurahi pamoja, sehemu ambayo tukikutana, hamu ya upendo na umoja inapanda zaidi.

Suala la kuonyesha uwezo uwanjani, tuwaachie Simba, uongozi wao na benchi la ufundi. Wao ndio wanajua wamejipanga vipi. Lakini tukumbuke, Infantino na Motsepe hawataangalia mpira pekee.

Badala yake wataangalia kila sehemu ya uwanja na moja wapo ni katika majukwaa ambako ni moja ya sifa kubwa ya Tanzania.

Simba walianza kujizolea sifa hii kwa muda mrefu wakijaza watu wengi katika mechi zao na baadaye Yanga nao na hasa msimu uliopita, wakaowanyesha Caf kuwa nao ni wazima hasa katika suala la mashabiki.

Sasa ni wakati wa michuano hii mikubwa mipya na wametupa nafasi ya kufanya uzinduzi, wanajua Tanzania na mpira ni damudamu.

Tuwaonyeshe hatujakosea na tuwaonyeshe sisi na mpira ni amani na upendo na ndio sehemu ya mtoko ambayo inaheshimika.

Kumbukeni 2027, tutakuwa na Afcon. Hii maana yake kuja kwao pia ni sehemu ya ukaguzi. Hii maana yake ni lazima tuwe makini katika mambo mengi kutokana na ugeni huo mkubwa tulioupata na tuutumie vizuri kwa kuwa watoa maamuzi katika mpira wa dunia na Afrika, watakuwa nasi jukwaani kuishuhudia Simba wakicheza dhidi ya vigogo wa Afrika, Al Ahly.