MPANGILIO wa ratiba ambayo inapangwa na Bodi ya Ligi Tanzania umekuwa ukienda kwa kasi kutokana na mashindano ambayo yapo.
Tunaona mzunguko wa tatu umekwenda kwa umakini na kilatimu kukamilisha majukumu yake. Ni mzunguko wa nne sasa huku kila timu ikipambana na hali yake.
Jambo la msingi kwa wachezaji na benchi la ufundi kuwa tayari kwa ajili ya mechi zote ambazo zinapangwa. Timu ambazo zinashiriki mashindano ya kimataifa hizi nazo zinapaswa kuheshimu ratiba inayopangwa.
Muda wa kulalamika kuwa ratiba inabana, safari ni ndefu kwa timu unapaswa uwekwe kando na badala yake nguvu kubwa iwe kwenye maandalizi.
Kila kitu kipo wazi kuhusu ratiba, kwa wapangaji wa ratiba wanatambua ugumu uliopo na wepesi wake kwa namna ya kupanga.
Hakuna anayependa kumuumiza mtu kwenye upangaji wa ratiba kila mmoja anajitahidi kutimiza majukumu yake anayofanya.
Malalamiko huwa yanaanza pale timu inapoondoka nyumbani na kupata safari kueleka sehemu nyingine, muhimu kutambua kwamba hata wao kuna mechi ambazo huwa wanacheza nyumbani.
Miundombinu ya Tanzania inazidi kuimarika kila leo hivyo suala la umbali linazidi kupungua taratibu. Kikubwa ni maandalizi mazuri kwenye kila mchezo.
Ratiba ipo na kubadilika ni jambo la kawaida kutokana na umuhimu wa matukio yaliyopo mbele. Lakini ni muhimu mpangilio wa ratiba nao ukawa ni rafiki kwa timu zote iwe ni Championship, Ligi Kuu Bara na mashindano mengine.