WAKIWA wameandika rekodi ya kutwaa mataji matatu msimu wa 2022/23 Yanga wameweka wazi kuwa wanajipanga kuvunja rekodi hiyo.
Ni Ngao ya Jamii Yanga walitwaa kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba, walitwaa ligi na Azam Sports Federation kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa fainali, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Katika anga la kimataifa Yanga waligotea nafasi ya pili katika Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa ni mashuhuda wa USM Alger kutwaa taji hilo kubwa Afrika.
Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga alisema kuwa mwanzo wa msimu mpya wanahitaji kuendelea na kasi ya kutwaa makombe zaidi.
“Tunahitaji kuendelea kutwaa mataji kwa kuwa furaha ya timu ni kutwaa mataji hilo linawezekana ikiwa tulitwaa Ngao ya Jamii, ligi kisha Azam Sports Federation bado tuna nafasi ya kutwaa kwa mara nyingine.
“Kinachofanyika kwa sasa kwenye kila mchezo wachezaji wanatambua ni muhimu kujituma na kupambana kupata matokeo mazuri mwisho itakuwa ni kufikia malengo yetu,” alisema Kamwe.
Agosti 9 Yanga inatarajiwa kumenyana na Azam FC katika mchezo wa Ngao ya Jamii hatua ya nusu fainali ya kwanza Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.