SIMBA UNYAMA NI MWINGI MPAKA UNAMWAGIKA

“HISTORIA mpya imeandikwa kwa tiketi zote kununuliwa siku tatu kabla ya SIMBA DAY. Shukrani kwa mashabiki wote ambao wamenunua tiketi.” Hii ni taarifa fupi ambayo ilitolewa na Simba Alhamisi kuelekea kilele cha tamasha lao kubwa Agosti 6 2023.

Yamebaki masaa tu, kabla ya tukio hilo kubwa na la kihistoria ambapo uongozi wa Simba umebainisha kuwa nchi itasimama kutokana na tukio hilo na sapraizi kubwa zitakazotangazwa kwa Uwanja wa Mkapa.

Tayari Yanga wamekamilisha utambulisho wa wachezaji wao pamoja na benchi la ufundi kwenye SportPesa Wiki ya Mwananchi na Singida Fountain Gate wao ilikuwa Singida Big Day.

Hapa tunakuletea kwa ufupi dondoo muhimu kuhusu tamasha hilo ambalo linatajwa kuwa habari kubwa na inayofuatiliwa zaidi nchini kwa sasa kama ifuatavyo;

Historia fupi ya Simba Day

Ni miaka 14 sasa imepita tangu kuanzishwa kwa tukio hili kubwa na la kihistoria mwaka 2009, ambapo kesho Jumapili tamasha hilo litafanyika kwa mara ya 15.

Tukio hili huashiria kufunguliwa rasmi kwa msimu mpya ndani ya klabu ya Simba, ambapo wadau wote wa timu hiyo kuanzia viongozi, benchi la ufundi, wachezaji, wanachama na mashabiki hukutana kwa pamoja kwa ajili ya kufurahia burudani mbalimbali.

Kunakuwa na utambulisho rasmi wa kikosi cha msimu husika ambao husindikizwa na burudani za muziki na mambo mbalimbali kabla ya kuhitimishwa kwa mchezo wa kirafiki.

Rais Dkt. Samia ndani ya nyumba

Katika kuonyesha kuwa wamedhamiria kufanya tukio kubwa na la kihistoria Simba wametangaza kuwa wanamtarajia Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu kuwa mgeni rasmi.

Ni taarifa yao rasmi iliyotolewa Ijumaa ilieleza: “Karibu kwenye kilele cha Wiki ya Simba. Karibu kwenye Simba Day, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hii ni siku muhimu kwa Klabu ya Simba na wapenda michezo wote nchini Tanzania.

“Tunakushukuru na tanakukaribisha kwa furaha kubwa isiyo na kifani. Kwa kipekee kabisa, tunakushukuru sana kwa mchango wako mkubwa kwenye sekta ya Michezo na Maendeleo ya Taifa kwa ujumla. Karibu sana Mheshimiwa Rais.”

Baada ya Diamond Platnumz sasa King Kiba

Miongoni mwa matukio ambayo yanatarajiwa kuacha gumzo kubwa kwenye tamasha la Simba Day Jumapili ni shoo kali ya msanii wa muziki, Ali Kiba lKing Kiba’ ambaye alitangazwa rasmi kuhamia Simba akitokea kwa watani zao wa jadi Yanga.

King Kiba tayari ameachia nyimbo kali ya Simba ambayo inasumbua kwenye majukwaa mbalimbali ya muziki hususani kwenye mtandao wa YouTube.

Ali Kiba kuhamia Simba imetafsiriwa na mashabiki wengi kuwa ni majibu kwa watani zao wa Jadi Yanga ambao Juni 13, mwaka huu walitangaza kumkaribisha msanii Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye alikuwa Simba.

Katika biashara ya muziki, wasanii hao wawili wanatajwa kuwa na ushawishi mkubwa zaidi hapa nchini, hii inakuwa historia mpya kwa Simba kufanikiwa kupandisha wasanii wakubwa wawili hapa nchini kwenye jukwaa la tamasha lao, ikumbukwe Diamond alitumbuiza Simba Day ya mwaka 2020.

Power Dynamos tena? mtego huo

Kama ilivyo kawaida Tamasha la Simba Day kwa kawaida hufungwa na mchezo wa kimataifa wa kirafiki ambapo mwaka huu watacheza na Power Dynamos ya Zambia.

Kwa wengi wanaamini huu ni mtego kwa Simba kwani huenda timu hizi zikakutana tena hatua ya kwanza ya Ligi ya mabingwa Afrika ikiwa Power Dynamos watavuka hatua ya awali. Nani atafaidika kumsoma mwenzake?

Lakini kama ulikuwa hujui, hii siyo mara ya kwanza kwa Powwer Dynamos kualikwa kwenye tukio la Simba day kwani mwaka 2019 walialikwa na kuambulia kipigo cha mabao 3-0 huku mabao hayo yote yakifungwa na Meddie Kagere.

Baada ya “Mlete Mzungu”, Luis kuiteka shoo?

Kupitia dirisha hili kubwa la usajili, Simba wametangaza mastaa wapya tisa na tukio linalosubiriwa kwa hamu ni utambulisho wa mastaa wapya, msimu uliopita kivutio kikubwa ni straika Mserbia, Dejan Manojlovic ‘Mlete Mzungu’.

Kwa msimu huu utambulisho wa mchezaji uliofuatiliwa zaidi mtandaoni ni wa, Luis Miquissone swali ni je, utambulisho wake utaiteka Shoo?

Uwanja utajaa saa 4?

Mwaka uliopita Simba walifanikiwa kujaza uwanja majira ya saa 7 mchana, msimu huu kupitia mitandaoni mashabiki wa timu hiyo wameweka wazi wanataka kuandika rekodi ya kujaza Uwanja wa Mkapa saa 4 asubuhi, yaani muda ambao mageti yanatarajiwa kufunguliwa.

Licha ya tiketi kuisha mapema, Matawi mbalimbali likiwemo Tawi la Simba Kibamba yanaendelea kuhamasishana kuhakikisha wanaandika rekodi hiyo, wataweza?

Simba wenyewe wanasemaje?

 Meneja wa Habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema: “Hili ni tamasha kubwa zaidi ambalo linakwenda kufanyika mwaka huu, ni tukio ambalo litaisimamisha nchi. Kuna burudani kubwa wataipata mashabiki wa Simba.

“Kila mmoja ameuona usajili mkubwa ambao tumeufanya, hii ni kwa ajili ya Burudani ya Simba Day na msimu wa makombe wanasimba hawapaswi kukosa tukio hili kubwa la kihistoria.”