MASTAA WAPYA YANGA SKUDU, MAXI WAPEWA MZIGO MZITO

ALIYEKUWA mshambuliaji wa Yanga, Mkongomani, Fiston Mayele, amesema anaamini usajili uliofanywa na timu hiyo, unatosha kabisa kutetea makombe yote ya ndani katika msimu ujao wa 2023/24.

Yanga ina kibarua kigumu cha kutetea makombe yake ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports ambayo mshambuliaji huyo alihusika kuyabeba msimu wa 2022/23.

Timu hiyo katika kuelekea msimu ujao wa 2023/24, imefanikiwa kuwasajili Pacome Zouzoua, Nickson Kibabage, Maxi Mpia Nzengeli, Kouassi Attohoula Yao, Gift Fred, Jonas Mkude, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ na Hafiz Konkoni.

Mayele amesema anaamini uwezo na ubora wa wachezaji wapya ambao wamesajiliwa na Yanga akiamini kama wakiingia katika mfumo zuri wa Kocha Mkuu Muargentina, Miguel Gamondi, basi watabeba makombe hayo sambamba na kufika mbali katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mayele amesema kuwa licha ya ubora huo, hawatakiwi kubweteka na badala yake kuongeza bidii ya mazoezi binafsi yatakayowafanya waongeze viwango vyao ili wawafuraishe mashabiki kwa matokeo mazuri ya ushindi.

“Kwa aina ya usajili ambao Yanga wameufanya, wanaweza kutetea makombe yote ambayo tuliyachukua mimi nikiwepo hapo.

“Nimeufuatilia usajili wa Yanga ambao wengi wachezaji nawafahamu akiwemo Maxi, ni kiungo mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao.

“Lakini niwaonye kuwa Ligi Kuu Bara ni ngumu, kwani timu nyingi zinaipania Yanga zinapokutana nayo, hivyo ni lazima wawe fiti kwa kufanya mazoezi mengi zaidi,” amesema Mayele ambaye ametimkia Pyramids ya Misri.