SPORTPESA NA SINGIDA FOUNTAIN GATE WAREJESHA KWA JAMII

SPORTPESA imeungana na Singida Fountain Gate FC kutembelea wodi ya Wamama Singida, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Singida katika maadhimisho ya Singida Big Day.

Ipo wazi kuwa SportPesa ni wadhamini wakuu wa Singida Fountain Gate FC iliyokamilisha jambo lao la Singida Big Day Agosti 2 2023 Uwanja wa Liti, Singida.

SportPesa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Abbas Tarimba pamoja na wawakilishi wa timu ya wanawake walifika hapo kuzungumza na wagonjwa na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa ajili ya wagonjwa.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo Tarimba alisema: “SportPesa kupitia Klabu ya Singida Fountain Gate tumeungana ili kuwafariji wagonjwa hawa ikiwa ni moja ya njia ya kuwafariji na kuwatia moyo wagonjwa wa Singida.

“Kilichotufanya tufike hapa ni udhamini wetu kwa timu ya Singida Fountain Gate kama mdhamini mkuu na tunajivunia maendeleo ya timu kwa msimu uliopita ikiwemo kufika tano bora katika Ligi Kuu Bara.

“Pia timu ya Singida Fountain Gate imepata nafasi ya kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa hili ni jambo kubwa kwetu kuwa karibu na jamii,”.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovik alianza kwa kuushukuru uongozi wa Singida Fountain Gate pamoja na SportPesa kwa moyo huo.

“Tumefurahi sana kuona mmetoka Dar kuja Singida kuleta misaada kwa wagonjwa hii ni ishara kuwa mnapenda maendeleo ya Singida licha ya kudhamini timu mnakuja kuwatazama na wagonjwa pia.”.