JONAS MKUDE APIGWA MKWARA YANGA

MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga amewapiga mkwara mzito mastaa wote wa timu hiyo ikiwa ni pamoja na kiungo Jonas Mkude aliyeibuka hapo akitokea ndani ya kikosi cha Simba.

Habari zinaeleza kuwa Gamondi kwenye uwanja wa mazoezi yanayoendelea AVIC Town aliwaambia wachezaji wake kuwa wanapaswa kucheza kwa utulivu na kuepuka kucheza faulo ambazo hazina ulazima.

Miongoni mwa nyota aliokuwa akiwatazama kwa ukaribu ni kiungo mkabaji Jonas Mkude anayefanya kazi kwenye eneo hilo na Zawadi Mauya huku wengine ikiwa ni Farid Mussa, Salum Aboubhakari, ‘Sure Boy’ kwenye eneo la kiungo ndani ya Yanga.

Mtoa taarifa amesema kuwa Gamondi kwenye uwanja wa mazoezi aliwaambia wachezajiwa Yanga wanapaswa kuwa makini na kila mpira unaokuwa mbele yao pamoja na kumsoma mpinzani.

“Kocha amewaambia wachezaji wote kuwa wanapaswa kuwa makini na mpira pamoja na mpinzani kwa kuwa wasipokuwa imara watacheza faulo ama kuchezewa faulo jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao pamoja na mpinzani.

“Anachohitaji ni kuona kila mchezaji anafurahia kile anachofanya kwa usahihi na kuepuka makosa yasiyokuwa na ulazima hasa anapopoteza mpira ama anapokuwa na mpira,” ilieleza taarifa hiyo.

Hivi karibuni, Gamondi alisema kuwa kwenye eneo la mazoezi huko mbinu zote zinafanyika ili wachezaji kutambua namna ya kusaka ushindi.

“Kila kitu kwenye mchezo wa mpira kinafanyiwa kazi eneo la mazoezi na ninafurahia kuona wachezaji wanaelewa kile ambacho wanafundisha tuna amini tutafanya vizuri,”.