ZIKIWA zinahesabiwa siku kabla ya tukio la kihistoria kwa Klabu ya Singida Fountain Gate tayari timu itakayocheza mchezo wa kirafiki imewekwa wazi.
Ni AS Vita ya DR Congo itakuwa na kazi ya kuwapa burudani wakazi wa Singida na vitongoji vyake kwenye mchezo unaotarajiwa kuchezwa Agosti 2,2023.
Siku hiyo itakuwa ni Singida Big Day ambapo wachezaji na benchi la ufundi la Singida Fountain Gate inayoshiriki Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika itakuwa ikifanya tamasha lake kubwa.
Ofisa Habari wa Singida Fountain Gate, Hussein Massanza amesema kuwa ni mechi yenye hadhi ya kimataifa itachezwa.
“Hii ni mechi kubwa yenye hadhi ya kimataifa na tunakwenda kufanya mengi mazuri kwa ajili ya msimu mpya 2023/24 hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Liti,” amesema Massanza.
Miongoni mwa wachezaji ambao wapo ndani ya Singida Fountain Gate ni Meddie Kagere, Joash Onyango, Bruno Gomes na Deus Kaseke.
Singida Fountain Gate ina kibarua cha kusaka ushindi kwenye mechi za kimataifa ambapo inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Itamenyana na JKU ya Zanzibar baada ya droo kuchezwa na miongoni mwa wachezaji wapya watakaotambulishwa ni pamoja na Yahya Mbegu.