WINGI WA MASHABIKI UNAWEZA KUWA FAIDA ZAIDI, FEDHA BAADAE

TAMASHA la hitimisho ya wiki ya Wananchi la Yanga wiki iliyopita, kwa hesabu limefeli. Halikufikia kile kiwango ambacho kilikuwa kinatakiwa.

Halikufikia kwa kuwa kiwango cha watu kilichoingia kilikuwa kidogo kuliko ilivyotarajiwa na gumzo kubwa likawa ni tamasha hilo kukosa mashabiki wa kutosha.

Wiki moja kabla ya tamasha hilo kufikia, gumzo lilikuwa ni namna ambavyo maandalizi yalionekana yamepooza na hakukuwa na shamrashamra zozote kuelekea tamasha hilo ambazo zingeashiria kuna jambo linafuatia.

Ukweli ukaonekana na baada ya tamasha, mjadala ukawa ni kudorora kwake, idadi ndogo ya watu na wengi wakaanza kutafuta sababu na majibu sahihi ya kufanya watu wasijitokeze kwa wingi.

Wakati hayo yote yakitafutwa, wengi sana wakakwama kwenye sababu ya kiingilio na hasa kiingilio cha Sh 10,000 ambacho kilionekana kuwa sababu ya wengi kushindwa kwenda.

Binasfi nakubaliana na kusema kiingilio ni kikubwa lakini nakaa upande mwingine kusema kwamba kukosekana kwa mpangilio mzuri wa kulitangaza tamasha kulichangia likose watu.

Sh 10,000 unakwenda kuona mechi mbalimbali, wachezaji wapya, mechi ya kwanza ya kocha mpya na wasanii kadha wa kadha wakitumbuiza. Kweli kinaweza kuwa kiasi kikubwa hivyo?

Ungeweza kulipa kiasi hicho kwa kuhudhuria shoo ya Marioo pekee ambaye siku hiyo alikuwa ndani ya tamasha hilo na mambo mengine mengi.

Lazima tukubali suala la kuzipa klabu zetu thamani hasa zinapokuwa na jambo. Tukianza kuamini kila kitu kwenye bei rahisi basi tusiwe na matarajio makubwa ya klabu zetu hasa katika suala la thamani.

Klabu kubwa ina watu wakubwa, wenye nia za juu zaidi kuzifanya ziwe kubwa zaidi. Kuanza kuamini 5,000 ndio saizi ya klabu yako nayo ni shida.

Nimemsikia kiongozi mmoja wa Yanga akisema lengo lao lilikuwa ni kupata kiasi fulani cha fedha na si kujaza uwanja kama ambavyo wengi wamekuwa wakisema kuwa wameshindwa.

Kauli hiyo ndio imenifanya kuandika makala haya kwa lengo kuwakumbusha viongozi ingawa niliamua kuanza na kuwakumbusha mashabiki kwanza.

Kwamba unataka fedha na si watu, yes fedha ni muhimu lakini umuhimu unaanzia kwa watu kwa kuwa hawa ni muhimu zaidi na ndio wanaoleta hizo fedha.

Kama malengo ya fedha kwamba unataka kuingiza kiasi fulani, maana yake unalenga kuwa na watu kiasi fulani. Watu ndio wanaoleta hizo fedha lakini pia nguvu ya klabu ni watu.

Watu hao ndio wanaoleta watangazaji mbalimbali ambao watamwaga mamilioni au mabilioni ya fedha katika klabu kwa kuwa wadhamini huangalia kwenye watu wengi au mwenye watu wengi wakajitangaze.

Ukiangalia wadhamini wote wale mfano wa Sportpesa, walichokifuaya Yanga ni watu na si vinginevyo.

Unapokuwa na hadhira yenye watu wa kutosha na kuwafanya wadhamini waone ni sehemu zaidi ambayo watafanya nayo kazi kwa kupata manufaa ya hao watu.

Sasa kama wewe utakuwa unataka fedha na kusahau watu, basi ukumbuke hesabu zako ni mbovu. Watu ndio wanaotengeneza huo ukubwa wa klabu na kufanya watu wengi zaidi wajitokeze kufanya nayo kazi.

Kuna mambo mengi sana ya kujifunza hap ana uongozi wa Yanga unapaswa kukiri kwamba kuna makosa iliyafanya msimu huu ndio maana tamasha lake lilakosa watu kama ilivyokuwa imezoeleka.

Hii si nzuri na inapotokea wadhamini wameongezeka halafu watu wanapungua basi lazima mjue kuna jambo linapaswa kurekebishwa ili kuyaweka mambo sawa.

Kama ni maoni yangu, ningewakumbusha Yanga kuacha kufanya mambo kwa mazoea. Hakukuwa na uchunguzi wa mahitaji ya mashabiki kabla ya msimu kwisha na kabla ya tamasha.

Hakukuwa na wale ambao waliingia mtaani kuwakumbusha mashabiki kwamba kuna jambo lao siku fulani. Huenda ndio ile dharau ya suala la “Kispika” hakina lolote lakini tumeona mambo yamekuwa tofauti na kwa kifupi inaweza kuwa ni sehemu ya hasara.

Kama watu wangefuatwa, sidhani kama Yanga inakosa watu 30,000 au zaidi wa kulipa Sh 10,000 kuingia uwanjani kwa ajili ya tamasha lao pendwa.

Kwa kuwa ilionekana “watakuja tu” au “Unajua Yanga ni kubwa”. Tatizo ndio likaanzia hapo na mambo yakawa mabaya na mwisho unaona, nguvu inaanza kutumika tena kumwaga kila aina ya maneno ili ionekane klabu ndio ilitaka hivyo na imefikia malengo yake, jambo ambalo hata mtoto mdogo ataona ni uongo.

Wakati mwingine kukubali makosa kunatengeneza uwezo bora zaidi wa kurekebisha makosa badala kuendelea kulazimisha kuonekana licha ya kufeli, ndicho mlichokitaka.

Imeandikwa na Saleh Jembe.