LEO NI LEO ASEMAYE KESHO HUYO NI MUONGO

LEO ni leo mashabiki wa Yanga wapo ndani ya Uwanja wa Mkapa kushuhudia mastaa wao wapya na wale ambao walikuwa na kikosi hicho kwa msimu wa 2022/23.

Balaa la usajili Yanga bado wanaendelea nao wakishusha wachezaji wazawa na wale wa kigeni kuboresha timu hiyo iliyokuwa kwenye mwendo bora 2022/23.

Hapa tunakuletea baadhi ya mastaa waliopo kwenye utambulisho rasmi wa Yanga wakiungana na Kocha Mkuu, Migueli Gamondi mrithi wa mikoba ya Nasreddine Nabi ikiwa ni maingizo mapya pamoja na mpangilio wa matukio ya namna hii:-

Mataji

Yanga wana mataji matatu waliyosepa nayo msimu wa 2022/23 ikiwa ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Azam Sports Federation ni miongoni mwa yatakayozungumziwa Wiki ya Mwananchi.

Ikumbukwe kwamba ni hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika iligotea hivyo hesabu zao ni kuvunja rekodi kwa msimu wa 2023/24 ila itakuwa ni kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nahodha ni mzawa Bakari Mwamnyeto ambaye yupo na timu huku kipa mdaka mishale Djigui Diarra akiwa na uzi wa Yanga.

Burudani

Sehemu ya utambulisho haikosi burudani na huenda wasanii wa Bongo Fleva, filamu pamoja na wale wa maigizo bila kusahau Dj wakali watapata nafasi ya kutoa burudani kwenye Wiki ya Mwananchi iliyopewa jina la Imeendaaaaa.

Hawa ni mastaa wapya

Kibabage

Julai 5 nyota wa kwanza alitambulishwa ndani ya kikosi cha Yanga anaitwa Nickson Kibabage kutoka Singida Big Stars ambayo kwa sasa inaitwa Singida Fountain Gate.

Tayari mzawa huyo ameanza mazoezi na mastaa wengine walioweka kambi pale AVIC Town, Kigamboni.

Fred

Julai 11, Gift Fred alitambulishwa ndani ya Yanga kwa dili la miaka miwili akitokea SC Villa ya Uganda yeye ni beki. Anaungana na Zawadi Mauya ambaye ni kiungo.

Mkude

Julai 12 Jonas Mkude yeye ni kiungo mzawa ambaye atakuwa na uzi wa Yanga msimu wa 2023/24.

Kiungo huyo alikuwa ndani ya Simba anaibuka hapo akiwa huru baada ya kukutana na Thank You ndani ya Simba.

Maxi

Julai 13 Maxi Mpia Nzengeli  alitambulishwa ndani ya Yanga akitokea kikosi cha Maniema ya Dr Congo anasubiriwa wiki ya Mwananchi kuonyesha makeke yake.

Yao

Yao Attohola Julai 15 alitambulishwa ndani ya Yanga yeye ni beki kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast.

Taibi

Taibi Lagrouni huyu ni kocha wa mazoezi ya viungo alitambulishwa Yanga Julai 17.

Skudu

Julai 19 saa sita usiku alitambulishwa kiungo kutoka Marumo Gallants ya Afrika Kusini yeye anatajwa kupewa jezi namba sita ni Mahlatse Manoka Makudubela.