UONGOZI wa Simba umeibuka baada ya kukamilisha suala la kiungo wake Mzambia, Clatous Chama aliyegomea kambi ya nchini Uturuki kwa kutamka kuwa hawakuwa na hofu ya nyota huyo kutimka kikosini mwao.
Hiyo ikiwa ni saa chache tangu kiungo huyo afikie makubaliano na klabu na kukubali kujiunga na kambi hiyo ya maandalizi ya msimu ujao iliyopo Uturuki.
Wakati kiungo huyo akiwa na mgomo huo, Yanga ilikuwa ikihusishwa kuwepo katika mazungumzo kwa ajili ya kumsajili kwa kumuwekea ofa nono iliyomshawishi kutua huko.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa uongozi haukuwa na hofu ya kiungo huyo kuondoka katika msimu huu kutokana na kubakisha mkataba wa mwaka mmoja.
Ally alisema kuwa, Wanasimba waondoe hofu ya kiungo huyo kuondoka katika msimu huu na ujao, kwani suala lake limemalizwa na uongozi na mwishoni mwa wiki hii atajiunga na kambi ya Uturuki.
“Kama uongozi wala hatukuwa na mashaka na hofu ya Chama kuondoka Simba na kwenda huko ambako kulikuwa kunatajwa.
“Ninaamini taarifa hii itawafanya mashabiki wetu kuwa na furaha tele, baada ya suala la Chama kumalizika kwa pande zote mbili kwa maana ya mchezaji na uongozi kufikia pazuri.
“Ilikuwa ngumu kwa Chama kuondoka Simba katika usajili huu mkubwa, kwani alikuwa na mkataba hivyo ngumu kuondoka licha ya hofu kubwa ilikuwa kwa mashabiki,” amesema Ally.
Tayari nyota huyo amejiunga na wachezaji wenzake Uturuki akiungana na Fabrice Ngoma ambaye alikuwa anashughulikia masuala ya vibali.
Ngoma naye alikuwa anatajwa kuwa kwenye rada za Yanga.