UONGOZI wa Dodoma Jiji umebainisha kuwa upo sokoni kimyakimya kwa ajili ya kuboresha timu hiyo na umekamilisha usajili wa nyota Idd Kipagwile aliyekuwa Polisi Tanzania.
Kwa sasa timu zote Bongo zinaendelea na usajili ikiwa ni Yanga ambayo imemtambulisha mzawa mmoja pekee Nickosn Kibabage mpaka sasa ambaye alikuwa ndani ya Singida Fountain Gate.
Mbali na Yanga pia Namungo FC wao wamemtambulisha Erasto Nyoni na wamezindua uzi mpya kwa ajili ya msimu ujao wa 2023/24.
Kipagwile anakuwa nyota wa pili kutambulishwa ndani ya Dodoma Jiji baada ya kumtangaza Mtenje Albano aliyekuwa anacheza Coastal Union.
Ofisa Habari wa Dodoma Jiji Moses Mpunga amesema kuwa hawana kelele nyingi bali wanafanya kazi kweli.
“Tumekamilisha usajili wa nyota Idd Kipagwile na ni moja ya wachezaji wenye uwezo mkubwa hivyo tuna amini kazi itakuwa kubwa uwanjani.
“Sisi hatuzungumziwi sana lakini kamati yetu ya usajili inafanya kazi kubwa na Kipagwile atakuwa ndani ya timu yetu kwa msimu mpya.
“Wachezaji wetu ambao tumewasajili na wale ambao tunaboresha mikataba yao wameanza kuwasili kambini tayari kwa maandalizi ya msimu ujao,” amesema.