MORRISON, BANGALA WATAJWA SINGIDA FOUNTAIN GATE

UONGOZI wa Singida Fountain Gate umesema kuwa wanatamani kuwa na kiungo Mkongomani Yannick Bangala na Mghana Bernard Morrison kwa ajili ya msimu ujao huku ukipanga kuweka wazi kila kitu hivi karibuni.

Wachezaji hao wanahusishwa kutua Singida Fountain Gate kwa ajili ya msimu ujao ambao wanacheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga tayari imetangaza kuachana na Morrison huku ikitajwa Bangala huenda ikamtoa kwa mkopo.

Mtendaji Mkuu wa Singida Fountain Gate, Olebile Sikwane alisema kuwa wanatamani viungo hao wawepo nao katika msimu ujao wakiamini wataongeza thamani ya timu hiyo.

Sikwane alisema kuwa hadi hivi sasa hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika kati ya viungo hao na Singida Fountain Gate.

Aliongeza kuwa hatima ya viungo hao kuichezea timu hiyo, itajulikana hivi karibuni mara baada ya taratibu kukamilika.

“Tunakwenda katika michuano mikubwa Afrika ya Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo tunatamani tungekuwa na viungo hao.

“Ipo wazi Morrison yupo katika kiwango kikubwa ni kati ya viungo ambao wangekuja kuifanya Singida Fountain Gate imara.

“Pia Bangala ni kati ya viungo bora hivyo tunaamini kuwa akipatikana yeye na Morrison watakuja kuipa thamani timu yetu,” alisema Sikwane.

Chanzo:Championi.