WAKATI Clatous Chama akiwa anatajwa kuwa kwenye hesabu za mabosi wa Yanga, Simba wameweka wazi kuwa hawana tatizo ikiwa watapata ofa nzuri kutoka kwa watani zao hao wa jadi.
Ikumbukwe kuwa, Chama ambaye ni mali ya Simba, ni kinara kwenye kutengeneza pasi za mwisho ndani ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2022/23 alipotengeneza pasi 14, huku akifunga mabao manne.
Kiungo huyo hakuwa kwenye msafara wa kikosi cha Simba kilichoibukia Uturuki Julai 12, 2023 kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa 2023/24 jambo lililoibua tetesi kuwa anahamia Yanga.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, amesema, ikiwa kuna timu inahitaji huduma ya Chama inabidi ifuate utaratibu na wao hawana tatizo kwenye suala la kuuza wachezaji.
“Sisi tunaamini kwenye kuuza na kununua wachezaji, hatuwezi kukataa ofa, ikiwa itakuja inamuhitaji Chama au mchezaji gani sisi tunazungumza na ikiwa itakuwa na manufaa kwetu tunafanya biashara.
“Ikiwa watani zetu wanahitaji saini ya Chama basi wanapaswa wafuate utaratibu, lakini ninaamini hawataweza kumnunua kwa kuwa bei yake ni kubwa sana, kama watamchukua bila utaratibu hiyo itakuwa ni kesi na watadaiwa fedha nyingi kwelikweli,” alisema Ally.