MSHAMBULIAJI HUYU MLANGONI YANGA

INAELEZWA kuwa Sudi Abdallah, ambaye ni raia wa Burundi, ndiye straika mpya anayekuja Yanga kurithi mikoba ya Mayele anayeondoka kwenda kucheza kwenye moja ya klabu huko Saudi Arabia.

Sudi mara ya mwisho Januari 12, 2023, aliuzwa na Klabu ya Al-Naft SC  ya nchini Iraq ambapo Julai 5 alijiunga na Klabu ya Kuching City ya nchini Malaysia inayoshiriki ligi kuu ya nchini humo.

Habari kutoka Yanga zimeeleza  kuwa, baada ya uongozi wa Yanga kukosa matumaini ya kumpata Mayele, waliamua kuingia mawindoni kisha wakamnasa mwamba Sudi Abdallah aliyekuwa na ufalme wa kutosha nchini Iraq.

“Tunamshukuru Mungu kwa kutupatia mbadala wa Mayele, ambapo sasa msimu ujao tuna uhakika tena wa kwenda kutamba na bonge la straika wa mabao na mkali wa kuchana nyavu.

“Jamaa amekubali kujiunga kwetu kwa dau la milioni 400 tu huku kila mwezi akiomba mshahara wa milioni 25, fedha ambayo ni nafuu zaidi kwetu baada ya kushindwa kumbakiza Mayele,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika kabisa.

Ikiwa Mayele ataondoka ndani ya Yanga nyota huyo anatarajiwa kupewa mikoba yake ndani ya kikosi hicho.