MAYELE ANASEPA YANGA, ISHU IPO HIVI

UNAAMBIWA sasa ni rasmi kuwa mshahara wa milioni 50 aliopewa Fiston Mayele unamhalalisha hatakuwa mchezaji tena wa Yanga msimu ujao baada ya kuomba kwenda kukipiga nchini Saudi Arabia huku Yanga wakilambishwa zaidi ya Bilioni 1.2 kama dau la usajili.

Mayele alijiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili kisha akaongezwa mmoja mwaka jana akitokea As Vita ya DR Congo.

Wakati Mayele akijiandaa kusepa, tayari Yanga wameshaanza kusaka mbadala wake na jicho lao limeangukia kwa straika mwili jumba, Sudi Abdallah raia wa Burundi.

Chanzo chetu cha uhakika kimeliambia Championi Ijumaa kuwa, Yanga wamewekewa mezani dola laki 5 (Sh bil 1.2) kama fedha ya kununua mkataba wa mwaka mmoja uliosalia kwa Mayele.

Mbali na hapo, Mayele mwenyewe amepewa Sh Milioni 400 kama fedha ya usajili na mshahara wa dola elfu 25 (Sh mil 60.7) kila mwezi.

“Kwa sasa ninaweza kukuhakikisha kabisa kuwa, Mayele anaondoka kwetu na ataenda kucheza huko Saudi Arabia ambapo amepata moja ya timu na imempa zaidi ya mshahara wa Sh mil 60 kila mwezi.

“Mshahara huo umekuwa ni mkubwa kwetu hivyo tumeshindwa kumbakiza kwani pia wamempa dola 200,000 (Sh mil 486.1) kama sehemu ya usajili wake, huku kwetu wakitupatia hiyo zaidi ya Bilioni moja ili tumuachie,” kilisema chanzo hicho.