ISHU ZA KISHIRIKINA ZISIPEWE NAFASI

TUKIWA tunaelekea kuanza msimu mpya wa mashindano imegeuka hali ya mazoea hivi sasa kwenye Ligi Kuu Bara na ligi za madaraja ya chini kila baada ya mizunguko kadhaa tumeshuhudia baadhi ya timu zikilimwa faini mbalimbali kutokana na vitendo vya kishirikina.

Hali hii imegeuzwa mazoea na hii ni kutokana na adhabu ambazo zinatolewa huenda haziziathiri timu husika moja kwa moja ndiyo maana vikekuwa vikijirudia mara kwa mara.

 Ni aibu kwenye ligi yenye udhamini wa zaidi ya shilingi bilioni 200 bado kuna timu zinaamini kwenye imani za kishirikina licha ya kuwa haziwasaidii chochote.

Kuna wachezaji wa Yanga ambao walikuwa kwenye sakata hilo jambo ambalo halipaswi kuwepo kwa msimu ujao ambao ni mpya.

Sio Yanga tu hata Simba kuna wachezaji waliwahi kukutwa na sakata hilo muhimu kuongeza uwekezaji kwenye kila idara na kuacha masuala ya ushirikina.

Suala hili limegeuka ugonjwa sugu ambao ni kama umekosa tiba licha ya Bodi ya Ligi kupambana kadri ya uwezo wao kuudhibiti.

Inasikitisha kuona mchezaji anakumbana na rungu la kukosa baadhi ya michezo pamoja na kutozwa faini kisa kujihusisha na mambo ya giza ambayo bila shaka yoyote ni upuuzi ambao hauna msaada kwa timu kupata matokeo.

Kwa mfano kwenye timu kubwa hususani Simba na Yanga vipo vikundi vya wahuni wachache ambao wamejivika majukumu ya kufanya mambo haya kwa kigezo cha kuipa timu matokeo tena jambo la kusikitisha na baadhi ya viongozi wanashiriki moja kwa moja.

Kama kweli juju zinasaidia timu kupata matokeo kwa nini timu zinagharamia makocha na maofisa wengine wa benchi la ufundi? Kwa nini asiletwe mganga kutoka Njombe au Shinyanga akakaa kwenye benchi awaongoze akina Kapombe, Morrison, Mayele na wengine kuipa timu matokeo?

Ifike mahala viongozi wa hizi klabu muwajibike na muache kushiriki haya mambo ambayo hayana faida kwa klabu zaidi ya kuiingizia klabu hasara kwa kuingia gharama ambazo hazina kichwa wala miguu.

Inasikitisha kuona Simba, Yanga au Azam na hata timu za madaraja ya kati zinapopata matokeo kuna vikundi vya wahuni wachache vinajinasibu kwamba wao ndiyo wameicheza mechi.

Hatuwezi kujisifia kuwa na moja ya ligi bora Afrika huku tunaona akina Gadiel Michael na Aziz Ki wanafungiwa kisa imani za kishirikina. Kila kukicha tunaona Yanga, Coastal, Geita, Simba na wengine wanakumbana na faini kutokana na timu kupita milango isiyo rasmi.

Uchawi ungekuwa unasaidia kwenye mpira ni wazi tungekuwa na makombe ya kutosha kama taifa kwenye michuano ya kimataifa. Kuna haja gani ya kuwalipa mamilioni ya fedha akina Chama na Mayele ikiwa tunaamini hirizi zinazipa matokeo timu zetu?

Ifike mahala tuachane na hizi imani za enzi za mawe za kale mpira ni sayansi hauhitaji mambo ya hirizi, ungaunga wala majimaji kwa ajili ya timu kupata matokeo.

Nitoe rai kwa Bodi ya Ligi ikiwezekana adhabu ziwe kali zaidi ikiwemo timu kupokwa alama hata kama ikishinda kama ikithibitika pasi na shaka kuwa imejihusisha kwenye imani za kishirikina ambazo ni wazi zinaharibu taswira ya ligi yetu.

Azam Tv, NBC na wadhamini binafsi wameweka fedha zao kuona mpira mzuri unachezwa na siyo mashindano ya hirizi na kumwaga dawa viwanjani.

Jikiteni katika kutengeneza mabenchi bora ya ufundi kwa kuajiri makocha wa viwango na wataalamu wengine, pia jikiteni katika kusajili wachezaji wa viwango huu ndiyo uchawi pekee ambao utawafikisha nchi ya ahadi na wala siyo kuruka mageti au kumwaga unga wa ndere viwanjani.