UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa utafanya usajili makini kwa ajili ya kuwa na kikosi imara kwa msimu wa 2023/24 kuendeleza ushindani.
Ipo wazi kuwa Julai Mosi dirisha la usajili lilifunguliwa na linatarajiwa kufungwa Agosti 31 hivyo ni muda wa kuongeza nguvu ndani ya timu hiyo.
Yanga tayari imeanza kufikia hatua ya kuachana na baadhi ya wachezaji wake ikiwa ni Bernard Morrison, Eric Johora, Tuisila Kisinda na Dickson Ambundo ambao kwa sasa wapo huru.
Ofisa Habari wa Yanga Ally Kamwe alisema kuwa wanatambua wanachotakiwa kukifanya katika usajili na hawana mashaka kutokana na mipango inavyokwenda.
“Kwenye usajili sisi tumejipanga na kila kitu kinakwenda sawa kuna wachezaji ambao wanakuja ikiwa ni maalumu kwa ajili ya kuwa na kikosi imara kwa msimu ujao hakika ni wachezaji haswa.
“Miongoni mwa nafasi ambazo tutasajili ni kiungo na huyu ambaye atakuja kufanya kazi katika kikosi chenye bahati na mataji. Hivyo kwa namna ambavyo tutaboresha kikosi chetu itakuwa ni suala la benchi la ufundi kujua nani ataanza kwa kuwa wote ni bora,” alisema Kamwe.
Yanga ni pointi 78 walimaliza nazo msimu wa 2022/23 waliposepa na ubingwa wa ligi huku Simba wakiwa nafasi ya pili pointi 75.