WINGA MPYA ATUMIWA TIKETI YA NDEGE NA MABOSI YANGA

FUJO za usajili zinaendelea kwa ajili ya msimu ujao ni baada ya Yanga kumtumia tiketi ya Ndege, winga wa Klabu ya AS Maniema Union ya DR Congo, Maxi Mpia Nzengeli.

Nzengeli ni kati ya wachezaji ambao walikuwepo katika mipango ya kusajiliwa na Yanga kwa ajili ya kuboresha kikosi hicho kwa msimu wa 2023/24.

Winga huyo anayetumia mguu wa kulia, anakuja kuchukua nafasi ya Mkongomani mwenzake, Tuisila Kisinda aliyekutana na ‘Thank You’ hivi karibuni akirejeshwa RS Berkane ya nchini Morocco.

Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wenye ushawishi wa usajili, winga huyo alianza maandalizi ya safari ya kutoka DR Congo na kutua nchini tayari kwa ajili ya kukamilisha dili lake la usajili.

Kiongozi huyo alisema kuwa, winga huyo alitumiwa tiketi hiyo ya ndege baada ya kufikia makubaliano mazuri ya kuja kuichezea Yanga kwa ajili ya msimu ujao.

Aliongeza kuwa Yanga haikukutana na ugumu katika kumpata winga, kutokana na yeye mwenyewe kuonyesha nia ya kujiunga na timu hiyo, akivutiwa na baadhi ya wachezaji Wakongo ambao ni Shaaban Djuma, Jesus Moloko, Fiston Mayele na Yannick Bangala.

“Maxi hadi kufikia leo (jana) alikuwa katika maandalizi ya kuanza safari ya kutoka DR Congo kuja hapa nchini Tanzania kwa ajili ya kukamilisha usajili wake wa kujiunga na Yanga.

“Na anakuja kusaini mkataba moja kwa moja, ni baada ya mazungumzo kukamilika kwa asilimia mia moja yaliyofanyika huko DR Congo baada ya kutumiwa mkataba na kuusoma.

“Hivyo mara baada ya kutua nchini, atasaini mkataba wa miaka miwili Yanga, tunaamini winga huyo anakuja kuwa gumzo hapa nchini kama ilivyokuwa kwa Mayele kutokana na ubora wake,” alisema kiongozi huyo.

Meneja wa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alizungumzia hilo la usajili kwa kusema: “Usajili wa wachezaji wote wapya umekamilika, kilichobakia ni kuwatambulisha pekee na kuanzia wiki hii tutaanza kutambulisha vyuma vipya.”