SIMBA wanatarajia kwenda Uturuki kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika na mashindano ya ndani ikiwemo Azam Sports Federation (FA) 2023/24.
Mataji hayo yote kwa msimu wa 2022/23 yalichukuliwa na watani zao wa jadi Yanga huku Simba ikipishana na mataji yote.
Yanga iligotea nafasi ya kwanza kwenye ligi ikiwa na pointi 78 huku Simba ikigotea nafasi ya pili na pointi 73.
Uongozi wa Simba unataka timu ipate utulivu zaidi wakati wa maandalizi na ndiyo maana wamechagua nchi ya Uturuki ambayo wanaamini itakuwa na utulivu wanaouhitaji.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally ametoa sababu nne ambazo zimefanya wao wachague kwenda Uturuki licha ya kuwa kuna nchi nyingine ambazo wangeweza kupata utulivu.
Ahmedy Ally amesema: “Kuhusu kambi ya Simba Uturuki. Maswali ni mengi kwa nini mnaenda Uturuki si mngebaki tuu kama wenzenu.
“Jibu ni kwamba hela ya kwenda Uturuki ipo tuu sio mpaka tuuze jezi. Pili timu ya inayoshiriki Super League lazima iwe tofauti na wengine.
“Tatu timu ya 9 kwa ubora Afrika lazima ifanye maandalizi sehemu kubwa kubwa. Nne wachezaji wetu wana hadhi ya Uturuki na Ulaya. Halafu watu wa Uturuki wamefurahi kusikia tunaenda wamesema tumelipa heshima taifa lao.”
Simba wanatarajia kuondoka mwanzoni mwa wiki ijayo kwenda Uturuki kwa ajili ya pre-season hiyo.
Wachezaji wa Simba ikiwa ni pamoja na Moses Phiri, Habib Kyombo,Ally Salim, Shomari Kapombe wapo Bongo na walianza kufanyiwa vipimo ikiwa ni sehemu ya maandalizi.