SIMBA YAPITA NA SAWADOGO MAZIMA

ISMAILI Sawadogo hatakuwa miongoni mwa nyota watakaokuwa katika kikosi cha Simba msimu wa 2023/24 baada ya kufikia makubaliano ya pande zote mbili kuachana.

Nyota huyo ni shuhuda watani zao wa jadi Yanga wakitwaa ubingwa huku Simba ikigotea nafasi ya pili.

Kiungo huyo hakuwa chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Roberto Oliveira kutokana na kutokuwa fiti kwa muda mrefu alipokuwa akipambania hali yake.

Alikuwa ni ingizo jipya ndani ya Simba katika dirisha dogo raia wa Burkina Faso ambapo timu yake ya mwisho kabla ya kuibukia Simba ilikuwa ni Klabu Difaa El Jadida.

Taarifa rasmi iliyotolewa na Simba Julai Mosi ilieleza namna hii:”Uongozi wa klabu umefikia makubaliano ya pande mbili ya kuachana na kiungo mkabaji Ismael Sawadogo,”.

Ni mechi tatu alicheza ndani ya ligi akitumia dakika 99 na mchezo wake wa kwanza ulikuwa dhidi ya Dodoma Jiji, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ubao uliposoma Dodoma Jiji 0-1 Simba bao lilifungwa na Jean Baleke.

Wachezaji wengine ambao nao hawatakuwa ndani ya kikosi cha Simba ni pamoja na Beno Kakolanya ambaye ni kipa, Jonas Mkude, Agustino Okra, Nelson Okwa, Gadiel Michael.