YANGA SC, imemtangaza Miguel Ángel Gamondi, kuwa kocha mpya wa timu hiyo akichukua mikoba ya Mtunisia, Nasreddine Nabi ambaye waliachana naye hivi karibuni baada ya mkataba wake kufikia tamati.
Gamondi raia wa Argentina, anajiunga na Yanga akiwa mzoefu wa kufundisha soka Afrika kwa zaidi ya miaka 20, huku muda wake mwingi akiutumia kufundisha timu za Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika.
Kocha huyo mwenye miaka 56, kabla ya kujiunga na Yanga, timu ya mwisho kufundisha ilikuwa Ittihad Tanger ya Morocco ambapo aliachana nayo Aprili 16, 2022.
Mzaliwa huyo wa Olavarría nchini Argentina, pia ana uraia wa Italia ambapo katika ufundishaji wake, anapendelea zaidi mfumo wa 4-2-3-1.
Akizungumza baada ya kutambulishwa rasmi, kocha huyo alisema: “Mambo Wananchi, mimi ni Miguel Angel Gamondi, kocha kutoka Argentina, nimefanya kazi zaidi ya miaka 20 katika soka la Afrika, nimefundisha timu kama Wydad Casablanca, Mamelod Sundowns, Chabab, Esperance.
“Nilipata mafanikio nikiwa na timu hizo, nina furaha kujiunga na timu kubwa ya Yanga, kwangu naweza kusema ni timu kubwa Afrika, yenye mashabiki wengi.
“Ninaamini tutafanya kazi vizuri na mashabiki, viongozi na wachezaji wote kwa jumla kuleta mafanikio zaidi.
“Nina furaha kujiunga nanyi na tutaonana muda si mrefu. Daima Mbele, nyuma mwiko.”