>

UMAKINI NI MUHIMU KWA SASA

TUNAONA timu zimeanza kuwaacha wachezaj wale ambao walikwama kufanya vizuri ama mikataba yao imegota mwisho hilo ni jambo linalohitaji umakini.

Sio wachezaji tu hata benchi la ufundi imekuwa hivyo kama ambavyo wamefanya Yanga, Azam FC na Simba.

Mbali na Yanga na Simba tunaamini bado zingine zitafuata kwa kuwa mwanzo wa msimu ni mwanzo wa mipango mipya.

Kila mchezaji anatambua kile ambacho alikifanya kwa msimu huu ambao umegota mwisho na kila mmoja kupata alichokivuna.

Kazi bado haijaisha kwa kuwa msimu mpya unakuja na kila mchezaji anatambua kwamba akipata changamoto mpya ni lazima apambane kutimiza majukumu yake.

Ukweli ni kwamba kila mmoja anapenda kufanya vizuri akipata kazi kwenye timu mpya hivyo kwa makosa ambayo yametokea msimu huu ni muhimu kila mmoja kufanyia kazi.

Kwa benchi la ufundi ambalo limetoa mapendekezo ya aina ya wachezaji wa kuachana nao na wale ambao watahitajika kuwa ndani ya timu ni muhimu kufuata mapendekezo yao.

Muhimu kufuata utaratibu kwa kuwa nyakati zinakuja na kupita na maisha lazima yaendelee licha ya kwamba hakuna anayeitambua kesho.

Ni muda mzuri wa kufanya tathimini nzuri kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi hii ni kwa upande wa viongozi kuangalia malengo ambayo yamefanyika.

Hakuna kusita kwenye kufanya maamuzi magumu lakini yenye manufaa kwa timu pamoja na yule ambaye atafikia makubaliano ya kuachwa ama kusajiliwa.

Iwe hivyo kwa kila mchezaji ambaye amepata dili jipya anahitaji kupata changamoto ni muhimu kwake kuanza mipango mapema kufuata utaratibu uliopo.

Mambo hubadilika huenda wale ambao wanapewa mkono wa asante bado wana kitu ambacho kingeongeza nguvu kwa wakati ujao watakapopewa nafasi.