NYOTA WENYE SIFA HIZI KUSAJILIWA SIMBA,KOCHA AMESEMA

ROBERTO Oliveira, Kocha Mkuu wa Simba ameweka wazi kuwa anahitaji kupata viungo wengine wawili wa kazi kwenye kikosi hicho ili kuongeza ushindani wa namba.

Timu hiyo imepishana na ubingwa ambao umekweda kwa watani zao wa jadi Yanga.

Sifa za nyota ambao anawahitaji ni kama ilivyo kwa kiungo mshambuliaji Sadio Ntibanzokiza mwenye mabao 10 na pasi 12 za mabao pamoja na kiungo mkabaji kama Mzamiru Yassin mwenye mabao mawili na pasi tano za mabao.

Oliveira jina lake limepenya kwenye orodha ya makocha watatu wanaowania tuzo ya kocha bora akiwa kwenye chungu kimoja na Nasreddine Nabi wa Yanga pamoja na Hans Pluijm wa Singida Big Stars.

Kwenye ligi imegotea nafasi ya pili na pointi zake ni 67 ubingwa umeelekea Yanga yenye pointi 74 na zote zimebakiwa na mechi mbili mkononi.

Ikumbukwe kwamba Simba imepishana na mataji yote iliyokuwa inawania kuanzia Ngao ya Jamii, ligi, Kombe la Azam Sports Federation, Ligi ya Mabingwa mpaka Kombe la Mapinduzi.

Oliveira amesema: “Kama ambavyo nilisema kuwa ninahitaji kuwa na wachezaji wawili wawili kila eneo kama Saido, (Ntibanzokiza) hatacheza basi anakuwepo mwingine atakayechukua nafasi yake.

“Ikiwa Mzamiru atakuwa hayupo sawa basi anakuwepo mwingine mwenye uwezo kama yeye ama awe zaidi lakini anakupa kile ambacho unahitaji na hilo litatufanya tuzidi kuwa bora zaidi,”.