IJUE SABABU YA MABAO 10 YA SIMBA KUWEKWA BENCHI

BENCHI la ufundi la Simba limeweka wazi kuwa sababu ya mtambo wao wa mabao Moses Phiri kujenga ushikaji na benchi ni kutokuwa fiti asilimia 100 baada ya kupata maumivu.

Kinara wa utupiaji ni Fiston Mayele wa Yanga ambaye ametupia mabao 16 kwenye ligi msimu huu wa 2022/23.

Phiri katupia mabao 10 kibindoni kwenye ligi akiwa ni namba moja kwa utupiaji upande wa Simba na ametengeneza pasi tatu za mabao.

Baada ya kupata maumivu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba alikuwa nje kwa muda akipambania afya yake na kwa sasa tayari amesharejea lakini bado hajawa na uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza.

Nyota huyo hakuanza kwenye mchezo wa Kariakoo dabi ubao wa Uwanja wa Mkapa uliposoma Simba 2-0 Yanga na kwenye mchezo dhidi ya Wydad Casablanca ambao ulikuwa ni wa Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Mkapa hakuanza kikosi cha kwanza.

Juma Mgunda, kocha msaidizi wa Simba amesema kuwa Phiri ni mchezaji mzuri lakini bado hajarejea kwenye uimara wake asilimia kubwa.

“Phiri ni mchezaji mzuri tangu alipopata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar bado hajarejea kwenye ule ubora wake hivyo taratibu anazidi kuimarika tuna amini atarejea kwenye ubora wake,”.