MZAWA Ayoub Lyanga anayekipiga ndani ya kikosi cha Azam FC ni mtambo wa mabao kutokana na kuhusika kwenye mabao mengi zaidi.
Lyanga ameanza kikosi cha kwanza kwenye mechi 15 akifunga mabao manne na ametoa pasi 7 za mabao moja kati ya hizo alitoa kwenye mchezo dhidi ya Yanga, Uwanja wa Mkapa.
Nyota huyo kahusika kwenye jumla ya mabao 11 ndani ya timu hiyo.
Bao lake la kwanza msimu wa 2022/23 aliwatungua Polisi Tanzania kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Ushirika, Moshi ilikuwa Desemba 5 2022.
Mabao yake mawili kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Jamhuri yanamfanya afikishe mabao manne kibindoni na pasi zake ni 7.
Azam FC inayonolewa na Kali Ongala baada ya kucheza mechi 27 safu yake ya ushambuliaji imetupia mabao 44 na kinara ni Idris Mbombo mwenye mabao 7 na pasi moja ya bao aliyompa Lyanga.
Kwenye msimamo ipo nafasi ya tatu imekusanya pointi 53 ni timu ya kwanza kuitunga Simba msimu wa 2022/23 iliposhinda bao 1-0 na itakutana nao kwa mara nyingine nusu fainali Kombe la Azam Sports Federation, Uwanja wa Nangwanda Sijaona.