BAADA ya Yanga kukamilisha kete ya kwanza ugenini, wawakilishi wa Tanzania kwenye anga la kimataifa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika wamerejea Bongo.
Kwenye mchezo huo uliochezwa nchini Nigeria baada ya dakika 90 ubao ulisoma Rivers United 0-2 Yanga na mabao yote yakifungwa na Fiston Mayele.
Tayari kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi kimerejea Dar na hesabu zao ni kuelekea mchezo wa robo fainali ya pili unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Jumapili.
Miongoni mwa wachezaji ambao wapo kwenye msafara huo ni pamoja na kipa namba mbili, Metacha Mnata, Djigui Diarra ambaye ni kipa namba moja, Khalid Aucho, Kibwana Shomari na Bakari Mwamnyeto.
Mara baada ya kuwasili Dar kikosi hicho kielekea moja kwa moja kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo ambao utatoa matokeo ya mwisho kwa timu itakayotinga hatua ya nusu fainali Kombe la Shirikisho Afrika.
Ally Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga ameweka wazi kuwa wapo tayari kwa mchezo ujao hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi.