NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga, amesema washambuliaji wake ikiwa ni Fiston Mayele na Kennedy Musonda wanapaswa kuongeza umakini kwenye kutumia nafasi wanazopata ili kufunga mabao mengi.
Yanga ni vinara wa Ligi Kuu Bara msimu huu, kibindoni wana pointi 68 baada ya kucheza mechi 26, tofauti ya pointi tano na watani zao wa jadi Simba wenye 63.
Akizungumza na Spoti Xtra, Nabi alisema kuna umuhimu kwa safu ya ushambuliaji kuongeza umakini na kutumia nafasi wanazopata kwenye kila mchezo.
“Unaona tumetoka kupoteza dhidi ya Simba, haina maana kwamba tulizidiwa sana, hapana, ilikuwa ni kushindwa kutumia nafasi ambazo tulipata hasa kipindi cha pili.
“Kipindi cha kwanza ukweli tulivurugwa hasa kwa kufungwa bao la mapema ambalo lilitokana na kona, kuna kazi ya kufanya kwenye mechi zijazo hasa kuhakikisha nafasi ambazo tunapata kwa washambuliaji wetu wanafunga,” alisema Nabi.
Kwenye mchezo uliopita Aprili 16, mwaka huu dhidi ya Simba, Nabi alianza na washambuliaji wawili, Mayele na Musonda ambao majaribio yao yote yaligotea kwenye mikono ya kipa namba tatu wa Simba, Ally Salim, mechi ikaisha kwa Yanga kufungwa mabao 2-0.