BALEKE, CHAMA KWENYE KAZI NYINGINE

CLATOUS Chama, Jean Baleke na Saido Ntibanzokiza baada ya kutimiza majukumu yao kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali wakishuhudia ubao wa Uwanja wa Azam Complex ukisoma Simba 5-1 Ihefu leo wana kazi nyingine kusaka ushindi.

Mchezo wa leo ni wa ligi unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Highland Estate ikiwa ni mzunguko wa pili ule wa mzunguko wa kwanza ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 1-0 Ihefu ilikuwa Novemba 22.

Chama alitoa pasi mbili kwenye mchezo uliopita wa robo fainali Kombe la Shirikisho huku Baleke akitupia mabao matatu, Ntibanzokiza na Pape Sakho hawa walitupia bao mojamoja.

 Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa baada ya kupata ushindi dhidi ya Ihefu kwenye mchezo wa Azam Sports Federation wachezaji wana kazi nyingine kusaka ushindi.

“Wachezaji wote baada ya mchezo wetu dhidi ya Ihefu kukamilika wanakazi nyingine kusaka ushindi kwenye mchezo wa ligi, mchezo ni mgumu na tunatambua ushindani uliopo hivyo kila mmoja ikiwa ni Chama, Baleke,Sakho,Kibu kazi ni moja kutafuta ushindi.

“Kikubwa Wanasimba wa Mbeya muhimu kuwa pamoja nasi na kuendelea kuishangilia timu yao kwani wao ni sehemu kubwa ya matokeo mazuri hivyo wajitokeze kwa wingi,” amesema Ally.

Kwenye msimamo Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 24 inakutana na Ihefu iliyo nafasi ya 6 pointi 33.