HIKI HAPA KILICHOWAPA JEURI YANGA MBELE YA WAARABU

NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa kilichoipa nguvu timu hiyo na kuongoza kundi mbele ya Waarabu wa Tunisia, US Monastri ni umakini wa wachezaji wote pamoja na ushirikiano.

Timu hiyo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika inaongoza kundi D na mchezo wake uliopita iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 US Monastri kete yao inayofuatwa ni dhidi ya TP Mazembe, Aprili 2.

Katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa ubao ulisoma Yanga 3-1 TP Mazembe hivyo mchezo ujao utakaochezwa DR Congo kila timu itakuwa na kazi ya kusaka pointi.

Nabi amesema kuwa wachezaji wamekuwa na juhudi kwenye kutimiza majukumu yao jambo ambalo linawapa matokeo.

“Ushirikiano ni mkubwa kwa wachezaji na kila mmoja anapenda kuona tunapata matokeo mazuri, kwenye mechi za nyumbani na ugenini tumekuwa tukifanya hivyo jambo ambalo linatufanya tuwe hapa tulipo.

“Bado kazi haijaisha kwa kuwa kila hatua moja tunayotoka kuelekea nyingine ni muhimu kuendelea kupata ushindi, mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi kwa kuwa wanatuongezea nguvu kwenye mechi zetu,” amesema Nabi.