UONGOZI wa Simba, umeweka wazi kuwa mitambo yao yote ya kazi katika kikosi hicho akiwemo Clatous Chama na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ ina kazi maalumu ya kufanya kuelekea mchezo wa ugenini dhidi ya Raja Casablanca.
Katika Kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika, Raja ni vinara wakiwa na pointi 13, kwenye mechi tano ambazo wamecheza hawajapoteza hata mmoja zaidi ya kuambulia sare moja, wameshinda nne.
Mechi nne walizoshinda, moja waliichapa Simba 0-3, Uwanja wa Mkapa, Dar. Timu hizo ambazo zote zimefuzu robo fainali, zitakutana kukamilisha ratiba.
Akizungumza na Spoti Xtra, Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, alisema: “Tunakwenda ugenini mchezo wa mwisho baada ya kumalizana na Horoya na kupata ushindi mkubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa hao Raja wanafuata lakini tutakuwa ugenini.
“Wachezji wetu akina Clatous Chama, Saidi Ntibazonkiza, Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute, hawa wana kazi kubwa ya kufanya ili kupata ushindi kwani hapo ndipo furaha yetu ilipo.”