MORRISON AANZA KUPIGA TIZI KWA SIRI

HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga, kuwa kiungo wao mshambuliaji Mghana, Bernard Morrison ameanza mazoezi ya binafsi ya siri kimyakimya.

Mghana huyo yupo nje ya uwanja kwa miezi miwili akiuguza maumivu ya nyonga ambayo aliyapata mara baada ya kurejea nchini akitokea kwao Ghana alipokwenda kwa ajili ya matatizo binafsi.

Staa huyo ameachwa katika msafara wa timu hiyo, uliosafiri kwenda nchini Tunisia kwa ajili ya mchezo wa hatua Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika watakaocheza keshokutwa Jumapili dhidi ya US Monastir.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, kiungo huyo alianza program ya mazoezi ya juzi Jumatano asubuhi kwenye moja ya gym jijini Dar es Salaam.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa program hiyo inakwenda sambamba na matibabu ndani ya wakati mmoja kuhakikisha anapona kwa haraka na kurejea kuipambania timu yake ya Yanga.

“Morrison ameanza mazoezi rasmi ya binafsi ya pekee akiwa chini ya uangalizi kwa hofu ya kujitonyesha na kurejesha maumivu yake ya nyonga.

“Juzi Jumatano alianza asubuhi program ya gym baada ya kupewa ratiba ya mazoezi na kocha wa fitinesi wa timu ambayo ataifanya kwa muda wa wiki tatu pekee kabla ya kuanza uwanjani.

“Hivyo ndani ya miezi hiyo miwili, Morrison atarejea akiwa fiti kwa asilimia mia moja kutokana na matibabu anayoendelea kuyapata,” alisema mtoa taarifa huyo.

Yanga kwa kupitia Meneja Habari na Mawasiliano wake, Ali Kamwe alizungumzia majeraha ya kiungo huyo na kusema kuwa: “Morrison hatakuwepo katika msafara wetu utakaokwenda Tunisia kutokana na maumivu ya nyonga.

“Tumemuacha kwa ajili ya kuendelea na matibabu ambayo ameyaanza na maumivu hayo ili kuhakikisha anakuwa fiti,” alisema Kamwe.