BALEKE AANDALIWA KUWAMALIZA HOROYA

KOCHA Mkuu wa Simba Mbrazil, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema kuwa mshambuliaji wake mpya Mkongomani, Jean Baleke yupo katika orodha ya wachezaji atakaowatumia katika mchezo wa kesho dhidi ya Horoya AC ya nchini Guinea.

Simba jana alfajili walisafiri kuelekea Guinea kucheza mchezo wao wa kwanza wa hatua ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya AC ya nchini huko.

Mkongomani huyo alitoa hofu ya kuwepo katika mchezo huo dhidi ya Horoya kutokana na majeraha ya enka aliyoyapata katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Robertinho alisema kuwa anafurahia ripoti ya madaktari aliyoipata imemruhusu kumtumia mshambuliaji huyo katika mchezo huo wa kimataifa.

Robertinho alisema kuwa, mshambuliaji huyo katika mazoezi ya juzi Jumatano asubuhi alifanya mazoezi mepesi, lakini katika program ya jioni aliungana na wachezaji wenzake kufanya magumu ya pamoja.

Aliongeza kuwa anafurahia uwepo wa mshambuliaji huyo akiamini ataiongezea nguvu safu yake ya ushambuliaji katika mchezo huo ambao muhimu kupata ushindi.

“Baleke ni kati ya wachezaji wangu tegemeo katika safu ya ushambuliaji, hivyo kurejea kwake kumenipa matumaini makubwa ya kufanya vema tutakapokuwepo ugenini kucheza dhidi ya Horoya.

“Kitu kizuri zaidi ana uzoefu wa mashindano haya, hivyo uwepo wake katika kutaongeza kitu tukiwa ugenini tukitaka ushindi pekee na sio kufungwa.

“Sakho (Ousmane) naye ana asilimia mia moja ya kumtumia katika mchezo huo, ni baada ya kupona majeraha ya enka aliyoyapata, alinipa hofu kubwa kuumia kwake,” alisema Robertinho.

Wakati huohuo, kiungo mshambuliaji wa Simba, Pape Ousmane Sakho alisema: “Maandalizi yetu ni mazuri, malengo yetu ni kushinda ugenini tutapambana ili kufanikisha hilo.

“Tunajua haitakuwa mechi rahisi, tutakuwa ugenini lakini tupo tayari kwa mpambano na mashabiki wetu tunawaomba mtuombee ili tukatimize malengo.”