MAYELE AWATUMIA SALAMU NZITO RUVU, KITAWAKA LEO KWA MKAPA

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Mayele amesema kuwa atahakikisha kuwa anaisaidia timu hiyo kuibuka na ushindi katika mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting huku akitamani kufunga bao katika mchezo huo.

Yanga leo Jumatatu wanatarajiwa kuwakaribisha Ruvu katika mchezo wa ligi kuu unaotarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Mkapa, Dar.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mayele alisema kuwa anatamani kuona anaendelea kuisadia Yanga kufanya vizuri kwa kufunga mabao muhimu katika mchezo ambao anaamini ni muhimu kwao kupata ushindi ili kuendelea kuongoza ligi na kufanikisha malengo yao.

“Kama kawaida malengo yetu ni kuhakikisha kuwa katika kila mchezo tunaibuka na ushindi, hata mchezo huu dhidi ya Ruvu matarajio yetu ni kuona tunapata ushindi mzuri ili tuendelee kuongoza ligi.

“Kwa upande wangu binafsi natamani kuona kuwa naendelea kufunga mabao muhimu ili niendelee kuisaidia timu, naamini kila kitu kinawezekana hivyo mashabiki wa Yanga wanatakiwa kuja kutupa nguvu ya kupambana,” alisema Mayele