BAO la mapema lililojazwa kimiani na staa wa Namungo FC, Ibrahim Mkoko dakika ya 07 halikutosha kuifikisha timu hiyo kutoka bara hatua ya fainali.
Ni kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi 2023 hatua ya nusu fainali ambapo baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Amaan ulisoma Mlandege 1-1 Namungo.
Bao lililoweka usawa kwa Mlandege lilipachikwa na staa wao Bashima Saite dakika ya 45 na kuifanya mechi kuzidi kuwa na ushindani mkubwa.
Dakika 45 za kipindi cha pili ngoma ilikuwa nzito na mshindi alipatikana kwa mikwaju ya penalti ambapo ni Mlandege walishinda penalti 5-4.
Mlandege sasa wanakwenda fainali na wanakwenda kumenyana na Singida Big Stars ambayo ilitinga hatua ya fainali kwa ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Azam FC.
Fainali hiyo inatarajiwa kuchezwa Januari 13,2023ambapo bingwa mpya 2023 atajulikana.
Ikumbukwe kwamba Mlandege hawa waliwatoa kwenye reli mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi Simba wa kuwachapa bao 1-0 mchezo wa hatua ya makundi.