VITA kali leo Alhamisi itakuwa pale darajani ambapo miamba miwili ya soka itavaana kila mmoja akiwa na machungu yake baada ya kuanza mwaka vibaya.
Huu utakuwa ni mchezo wa Premier League kati ya Chelsea na Manchester City ambao walianza mwaka 2023 kwa kupoteza pointi mbili kila mmoja ndani ya ligi hiyo. Mchezo utapigwa katika Uwanja wa Stamford Bridge.
Hautakuwa mchezo rahisi hata kidogo hasa kwa Chelsea ambao ni wenyeji wakiwa wanapita katika kipindi kigumu kutokana na aina ya matokeo ambayo wamekuwa wakipata chini ya Kocha Graham Potter.
Chelsea na Man City watakutana kwa mara ya kwanza mwaka huu wa 2023 na Man City wataingia na rekodi bora katika mchezo huo kwani mechi zao tatu za mwisho zote wameifunga Chelsea.
Kwa msimu huu toka umeanza, Chelsea imekuwa haina mwendo mzuri ndani ya Premier League ikishinda mechi saba pekee kati ya 16 ambazo zimecheza.
Wakati wakiingia katika mchezo wa leo, kumbuka Chelsea ametoka kutoka sare na vibonde Nottingham Forest, huku Man City naye akitoka sare na Everton na kupunguzwa kasi ya kufukuzana na Arsenal ambao ndiyo vinara wa ligi hiyo.
Kwa maana hiyo, mechi hii ambayo itazikutanisha timu za big six vita itakuwa sio ndogo kwenye mchezo huu.
Ukiangalia kwa timu zote hizi mbili kila mmoja anaonekana kuwa bora na dhaifu katika maeneo tofauti.
Kwa Chelsea wao ni wazi eneo lao la ushambuliaji limekuwa butu ndiyo maana hata suala la kufunga mabao limekuwa shida kwa upande na ukiangalia katika mechi 16 wamefunga mabao 20 tu huku wapinzani wao Man City wao wakifunga mabao 44 na mabao 21 ya City yamefungwa na Erling Haaland pekee.
Chelsea wamefanya mabadiliko sana katika eneo lao la ushambuliaji kwa kuleta sura mpya, lakini tatizo la ubutu limeendelea kuonekana kikosini hapo.
Lakini katika eneo la ulinzi la Chelsea halina tofauti na sana Man City ambao safari hii safu yao ya ulinzi imeyumba msimu huu wakiwa wameruhusu mabao 16 na wapinzani wao Chelsea wakiwa na wameruhusu 18. Na hapa ndiyo unaona tofauti yao.
Chelsea ambao ni wenyeji wa mchezo huo watakuwa na kazi ya kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu muhimu na mchezo huu pia huenda ukatoa hatma ya Potter ndani ya Chelsea na hii ni kutokana na mwendo wa timu hiyo kwa sasa.
Lakini kumbuka huu ni mchezo muhimu pia kwa Man City kuhakikisha wanapunguza gepu la pointi kati yao na Arsenal baada ya kupoteza pointi mbili katika mchezo uliopita.
Lakini katika mchezo huu huenda staa wa Man City, Haaland akaendelea kuweka rekodi kwa kuvunja rekodi ya mfungaji bora wa msimu uliopita wa Premier League ambaye alifunga mabao 23.
Wakati timu hizi zikiwa na njaa ya kusaka matokeo dakika 90 zitaongea kama Potter atasalia na kibarua chake au Man City watapunguza gepu lao na Arsenal, tusubiri.
MECHI 10 ZA MWISHO WALIZOKUTANA MICHUANO YOTE
Man City 2-0 Chelsea
Man City 1-0 Chelsea
Chelsea 0-1 Man City
Man City 0-1 Chelsea
Man City 1-2 Chelsea
Chelsea 1-0 Man City
Chelsea 1-3 Man City
Chelsea 2-1 Man City
Man City 2-1 Chelsea
Chelsea 0-0 Man City
21
Haaland pekee amefunga mabao 21 Premier msimu huu, wakati Chelsea timu nzima ina mabao 20.
05
Man City imeshinda mechi tano za mwisho kati ya kumi dhidi ya Chelsea.
04
Chelsea imeshinda mechi nne za mwisho kati ya kumi dhidi ya Man City.