MBRAZIL AIFUMUA SIMBA, AWAWEKA MTEGONI MASTAA

KOCHA Mkuu mpya wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ raia wa Brazil, amewaweka mtegoni mastaa wa kikosi hicho, baada ya kuweka wazi kwamba, mkakati wake wa kwanza ni kumpa nafasi kila mmoja kuonesha uwezo wake, ili kuwafahamu nyota wote na kuandaa kikosi cha kwanza.

Juzi Jumanne, Robertinho alitangazwa rasmi kuwa kocha mkuu wa Simba akichukua nafasi ya Mserbia, Zoran Maki, aliyeondoka Septemba, mwaka huu.

Baada ya kuondoka kwa Zoran mwanzoni mwa msimu huu, Simba imeongozwa na Juma Mgunda ambaye kwa sasa atakuwa msaidizi wa Robertinho.

Kabla ya kujiunga na Simba, Robertinho alikuwa akihudumu ndani ya kikosi cha Vipers FC ya Uganda ambapo msimu uliopita alifanikiwa kushinda mataji mawili, Ligi Kuu ya Uganda na FA ya Uganda, huku pia akifanikiwa kuifikisha timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na Spoti Xtra, Robertinho alisema: “Ni kweli nitalazimika kutoa nafasi kwa kila mchezaji kuonesha uwezo wake kabla sijafanikiwa kuwa na kikosi changu cha kwanza, haya ni mazingira mapya, nakutana na wachezaji wapya.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya pamoja, inabidi mimi binafsi kuanza kuweka programu zangu na kuwapa muda wachezaji wazoee mbinu zangu, na mimi kuwafahamu vizuri ili kuwa na kikosi kamili.”