>

MAKUNDI TAYARI YAMESHAPANGWA, MAISHA YAENDELEE

KWENYE ulimwengu wa mpira kwa sasa kinachozungumzwa ni kuhusu makundi ambayo yamepangwa huko Misri ambapo wawakilishi wa Tanzania kila mmoja ameona atakayecheza naye.

Simba yupo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga yupo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, hapa kazi ipo hasa ukizingatia inapokuja suala la mashindano ya kimataifa ni lazima kila mmoja afanye kweli.

 Kundi D Yanga yupo na TP Mazembe, US Monastir ya Tunisia na Real Bamako ya Mali na Simba yeye yupo Kundi C ataungana na Vipers,Horoya na Raja Casabalanca.

Wapo ambao wameanza kutoa hesabu kwamba kuna timu nyepesi kwenye haya makundi na wapo ambao wanaamini kwamba kuna timu ambayo itakwama kutusua.

Ukweli ni kwamba baada ya makundi kupangwa maisha yanaendelea kama kawaida huku zile tambo ambazo zinatambwa kwa sasa muda wake unakuja.

Jambo la msingi kwa sasa ni kila timu kupanga kete kwa umakini ili watakapofikia hatua ya kuanza kucheza hizo mechi wapate matokeo mazuri.

Hakuna ambaye anapenda kuona wawakilishi wetu kimataifa wanagotea hatua ya makundi hapana kila mmoja anapenda kuona timu zetu zinafika mbali.

Hii inawezekana ikiwa kuanzia wachezaji na viongozi kila mmoja akatimiza majukumu yao kwa ajili ya mechi hizo ambazo zinatarajiwa kuanza mapema mwakani.

Kazi itakuwa kwa wachezaji kusaka ushindi na kila mmoja anajukumu lake kwenye kutafuta matokeo chanya muda wa maandalizi ni sasa na inawezekana.

Hatua moja kila wakati kwenye mechi hasa za nyumbani msingi mkubwa uwe kupata pointi tatu muhimu.