>

USAJILI WA MTIBWA SUGAR UPO HIVI

UONGOZI wa Mtibwa Sugar umesema kuwa kwa sasa unasubiri ripoti ya benchi la ufundi ili kufanikisha mpango wa kusajili wachezaji wapya.

Dirisha dogo la usajili linatarajiwa kufunguliwa wiki ijayo ambapo timu hupewa muda wa kuboresha nafasi ambazo wataona zinahitaji kuongezewa nguvu.

Miongoni mwa wanaosakwa ndani ya Mtibwa Sugar ni kwenye eneo la ushambuliaji pamoja na ulinzi.

 Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema kuwa baada ya kumalizana na Geita Gold wamerejea na sasa wanaanza kujipanga upya.

 “Mchezo wetu wa mwisho mzunguko wa kwanza tumemaliza dhidi ya Geita Gold ugenini na kupata sare ya kufungana mabao 2-2 hivyo kwa sasa tunasuiri ripoti ya benchi la ufundi kuifanyia kazi.

“Tumekusanya pointi 22 baada ya kucheza mechi 15 tukiwa kwenye nafasi ya sita hivyo kuna jambo ambalo tumeona, tukipata ripoti ya benchi la ufundi tutaona nini wamependekeza tufayie kwa ajili ya mzunguko wa pili.

“Mapendekezo ya mwalimu ambayo yatatolewa hayo tutafanyia kazi kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi chetu kwa ajili ya mzunguko wa pili,”.