BEKI mwandamizi wa Barcelona, Gerard Pique ametangaza kuachana mazima na timu hiyo baada ya kuitumikia kwa miaka 14.
Raia huyo wa Hispania alibainisha jambo hilo kupitia kipande cha video aliyoweka kwenye mitandao ya kijamii ambapo amesema kuwa mechi ya Jumamosi itakuwa ya mwisho ndani ya Camp Nou.
Pique alionyesha picha zake za zamani akiwa kijana katika kituo cha kukuzia vipaji cha Barcelona na alijiunga na timu hiyo mwaka 2008.
Nyota huyo mwenye miaka 35 amefanikiwa kucheza mechi zaidi ya 600 akiwa na Barcelona, katwaa mataji 31 ya ngazi ya klabu ikiwa ni manne ya Ligi ya Mabingwa na mataji manne ya La Liga.
Mwisho wa video alisema:”Nimekuwa nikisema kila mara kwamba baada ya Barcelona hakutakuwa na timu nyingine na hivyo ndivyo itakavyokuwa.
“Jumamosi hii itakuwa mchezo wangu wa mwisho Camp Nou. Nitakuwa shabiki wa kawaida, nitaiunga mkono timu.
“Nitapitisha mapenzi yangu ya Barca kwa watoto wangu kama familia yangu ilivyonifanyia. Nitakuona Camp Nou. Uishi muda mrefu Barca, daima,”