VIUNGO wa Yanga ikiwa ni pamoja na Aziz KI, Feisal Salum, Bernard Morrison, Khalid Aucho wamepewa kazi maalumu kuelekea kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa nchini Sudan, Jumapili, Oktoba 16,2022 saa 2:00 usiku baada ya ule uliochezwa Uwanja wa Mkapa,ubao usoma Yanga 1-1 Al Hilal.
Nasreddine Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa kila mchezaji ana jukumu la kutimiza kazi yake uwanjani ili kuipa timu matokeo.
Kazi kubwa kwa viungo hao ni kutengeneza nafasi nyingi kuelekea lango la wapinzani ili washambuliaji wa timu hiyo wafanikiwe kufunga.
Ikumbukwe kwamba Nabi amekuwa akipenda kumtumia mshambuliaji Fiston Mayele mwenye mabao 7 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye hatua ambayo Yanga ipo.
Nafasi yake imekuwa ikichukuliwa na Heritier Makambo ambaye amekuwa na nafasi finyu kikosi cha kwanza msimu huu wa 2022/23.
Kazi nyingine ambayo wamepewa viungo hao ni kuhakikisha wanatumia mapigo huru kwa umakini ikiwa ni pamoja na kona pamoja na faulo ambapo jukumu la kupiga kona limekuwa likimuangukia kiungo Aziz KI.
“Tuna mchezo mgumu mbele yetu ambao ni dhidi ya Al Hilal, kwenye mpira wa miguu kila kitu kinawezekana na ambacho kinatakiwa kwa sasa ni kila mchezaji kutimiza majukumu yake.
“Ninajua kuhusu uwezo wa viungo ambao wapo pamoja na washambuliaji, muhimu kwenye nafasi tutakazopata kuzitumia kwani kwenye hatua za Ligi ya Mabingwa huwa zinapatikana nafasi chache ambazo ni muhimu kuzitumia,”.